DODOMA YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA MSISITIZO WA KUJIKWAMUA KIUCHUMI KUPITIA MIKOPO NAFUU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, March 8, 2026

DODOMA YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA MSISITIZO WA KUJIKWAMUA KIUCHUMI KUPITIA MIKOPO NAFUU


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule,amesema Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza kwenye kuwainua Wanawake
kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo ya 10% kutoka kwenye Halmashauri.Mhe Senyamule
ameyasema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani,zilizofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mbande,Wilaya ya Kongwa, ambapo
alikuwa mgeni rasmi.


“Katika Mkoa wa Dodoma mwaka 2024-2025, Mkao uliweza kutoa takriban shilingi
9,487,369,909 kama mikopo ya 10% kwa ajili ya wanawake lakini kupitia PPRA, ipo sheria
inayotaka Serikali ifanye kazi na makundi maalum wakiwemo wanawake ambapo vikundi
zaidi ya 500 vimeweza kufanya biashara na Serikali na zaidi ya Bilioni 16 zimelipwa kwa
wanawake walioweza kufanya biashara na Serikali”

Aidha, Mhe. Senyamule ametoa wito kwa wanawake wajasiriamali wadogo wajitokeze
kujisajili kwa ajili ya kupata vitambulisho ili wafaidike na fursa za mikopo inayotolewa na
Benki ya NMB kwani mpaka sasa Mkoa umesajili wajasiriamali wadogo wanawake 2,716
sawa na 8% ya wanaotakiwa kusajiliwa na wameweza kunufaika na mikopo ya Shilingi
Milioni 403.

Kadhalika, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ambaye ndiye mwenyeji wa Maadhimisho hayo
amesema Serikali imefanya kazi kubwa ya kupunguza vifo vya Mama na Mtoto kutokana na
kuongezeka kwa miradi ya uboreshaji afya ya uzazi ambapo mwaka 2021, Wilaya yake
ilikua na vituo vya afya vinne lakini kutokana na dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kupunguza vifo hivyo, ndani ya miaka mitano amejenga vituo vya afya 7.

Nae, Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Asha Nyoni, amewaasa Wanawake kukimbilia fursa zinazotolewa na Mamlaka
za Kiserikali na Wadau wengine wa Maendeleo ambapo Wizara yake inashirikiana na
TAMISEMI kuhakikisha uratibu wa Mikopo ya 10% kwa ajili ya wanawake wanaoamua
kujikwamua kimaendeleo inawafikia lakini pia Wizara inatoa mikopo ya 7% kwa
wanawake wajasiriamali ikiwa ni pamoja na mikopo ya ‘Women Development Fund’
inayotolewa moja kwa moja na Wizara hiyo.

Akisoma risala ya siku hiyo mbele ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji
Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Dodoma Bi. Mary Mabhaya ameiomba Serikali ya Mkoa
kusimamia masharti ya mikopo kwenye Taasisi za kifedha iendelee kupunguzwa ili kuokoa
gharama wanazoingia Wanawake katika ufuatiliaji wa mikopo hiyo.


Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoa wa Dodoma, yamehusisha washiriki
zaidi ya 6000 walioungana kutoka kwenye Wizara na Taasisi za Serikali zinazopatikana
Mkoani hapa sambamba na Wadau mbalimbali wa Maendeleo ya Jamii wanaojishughulisha
na masuala ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kama vile ''Aga Khan Foundation" na Benki
ya Azania ambao pia wamedhamini shughuli hiyo.












No comments:

Post a Comment