
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka Machi 8, wanawake wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) wametoa msaada wa mifuko 50 ya saruji, matofali 1,000 pamoja na mahitaji mbalimbali ya watoto katika Kituo cha kulea watoto yatima na waliofanyiwa ukatili cha Shalom kilichopo Kidenge B, Kata ya Msangani, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani Machi 6, 2026.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi msaada huo, Meneja wa Udhibiti na Viwango wa Mamlaka hiyo Bi. Sultana Seiff, alisema kuwa wanawake wa e-GA wameamua kusherehekea siku hiyo kwa kuwafikia watoto wanaohitaji msaada katika jamii na kukichagua kituo hicho ikiwa kama sehemu ya kurudisha kwa jamii.
Meneja huyo alisema kuwa baada ya kuwasiliana na kituo hicho na kupata changamoto mbalimbali zinazohitaji kutatuliwa katika kituo hicho ikiwemo ujenzi wa uzio ili kuhakikisha Watoto hao wanakua salama waliamua kuchangia vifaa vya ujenzi pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa Watoto hao.
“Napenda kuwasilisha salamu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa e-GA ambaye ametuwezesha wanawake wa Mamlaka hii kufika hapa Kibaha katika kituo hiki na kukabidhi mahitaji haya muhimu kwa ajili ya watoto na kituo hiki cha Shalom,” alisema Seiff.
Aliongeza kuwa mbali na vifaa vya ujenzi, pia wametoa mahitaji mengine muhimu ikiwamo chupi za kuzui mkojo kwa Watoto yaani pampers, maziwa ya watoto wachanga, sukari na mahitaji mengine ya msingi kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Kwa upande wake, mbeba maono wa kituo hicho, Bi. Lilian Mbise, aliwashukuru wanawake wa Serikali Mtandao kujitolea kwao kufika na kuwaona Watoto hao pamojana na msaada huo muhimu waliotoa.
“Tunaishukuru sana Mamlaka ya Serikali Mtandao kupitia wanawake wake ambao wameamua kuacha shughuli zao na familia zao na kuja hapa kutuunga mkono. Msaada huu wa saruji na matofali utasaidia sana katika ujenzi wa uzio,” alisema Bi. Mbise.
Akikielezea kituo hicho alisema kuwa, kituo cha Shalom kilianzishwa Mei Mosi mwaka 2016, kikiwa na watoto wawili, lakini sasa kinahudumia watoto 66 wa kike na wa kiume yatima pamoja na wale waliofanyiwa ukatili wa aina mbalimbali, ambao hufikishwa kituoni hapo kupitia taratibu za kiserikali.



No comments:
Post a Comment