KATIBU MKUU DKT. MUYUNGI AKUTANA NA UJUMBE WA KITUO CHA UMAHIRI WA SAYANSI KUSINI MWA AFRIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 7, 2026

KATIBU MKUU DKT. MUYUNGI AKUTANA NA UJUMBE WA KITUO CHA UMAHIRI WA SAYANSI KUSINI MWA AFRIKA


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Kituo cha Umahiri wa Masuala ya Sayansi na Usimamizi Endelevu wa Ardhi kutoka Nchi za Kusini mwa Afrika (SASSCAL).

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Machi 06, 2026 Jijini Dar es Salaam, ujumbe huo ulifanya ziara kwa ajili ya kujitambulisha na kuwasilisha maombi ya ushirikiano baina yake na Serikali.

Kupitia mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo hicho Prof. Gabriel Miguel alieleza masuala mbalimbali ikiwemo muundo na shughuli za kituo na miradi iliyotekelezwa katika nchi wanachama.

Kwa mujibu wa Prof. Miguel ameeleza utaratibu wa kujiunga na mtandao wa kituo hicho kwa nchi wanachama unaobainisha fursa na faida mbalimbali ikiwemo mapambano ya mabadiliko ya tabianchi, usimamizi endelevu wa ardhi na uhifadhi wa mazingira.

Aidha ameeleza kuwa taasisi hiyo imeendelea kujenga uwezo wa kitaalamu katika masuala ya kiufundi, ujenzi wa miundombonu na programu za masomo ya elimu ya juu kwa wataalamu katika nchi wanachama.

“Kituo kimefanya tafiti za masuala ya kilimo hifadhi, bayoanuai, mifumo ikolojia na nishati mbadala na kuhakikisha matokeo ya tafiti hizi yanaakisi mipango ya maendeleo katika nchi wanachama” amesema Prof. Miguel.

Prof. Miguel ameeleza kuwa kituo hicho kimekuwa kikifanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Serikali, mashirika ya mazingira, wadau wa viwanda na taasisi za kikanda.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi amekishukuru kituo hicho kwa kufanya ziara Tanzania na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha uhifadhi endelevu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha Dkt. Muyungi alieleza dhamira dhati ya Serikali kujiunga na kituo hicho ambapo aliainisha vipaumbele na maeneo ya ushirikiano ambayo ni muhimu kuzingatiwa kulingana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

“Tunashukuru kwa ziara hii ambayo imekusudia kuimarisha wigo wa ushirikiano katika nyanja ya sayansi, hili ni jambo muhimu kwa Serikali ya Tanzania hususani katika kipindi hiki tunachoelekea katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya taifa 2050” amesema Dkt. Muyungi.

Dkt. Muyungi pia alitoa ushauri kuhusu umuhimu wa kuundwa kwa timu ya pamoja ya wataalamu kati ya kituo na wataalamu watakaopendezwa na serikali ili kujadili kwa kina kuhusu faida zitakazopatikana iwapo Tanzania itaridhia kujiunga na taasisi hiyo.

SASSCAL ni kituo cha utafiti kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi, tathimini ya mazingira na usimamizi endelevu wa mazingira. Nchi wanachama wa Kituo hicho ni Angola, Botswana, Namibia na Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment