Serikali imesema itaendelea kuimarisha elimu ya ujuzi na umahiri ili kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuhimili ushindani wa soko la ajira, huku ikilenga kuwafikia vijana 80,000 kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi ifikapo Juni 2027.
Akizungumza katika Mahafali ya 18 ya Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Furahika kilichopo Buguruni Malapa, Ilala jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Hafidh Ameir amesema vijana wanapaswa kuchangamkia program hiyo kwa kuwa inalenga kutambua, kuthibitisha na kurasimisha ujuzi walioupata kupitia uzoefu wa kazi, mafunzo kazini na njia nyingine zisizo rasmi za kujifunza.
“Kupitia Program hii hakuna ujuzi unaopotea kwa kukosa utambuzi rasmi. Niwasihi vijana wote wenye ujuzi mlioupata nje ya mfumo rasmi kujitokeza na kutumia fursa hiyo kurasimisha ujuzi wenu,” amesisitiza Mhe. Wanu.
Amesema Serikali inaweka mkazo katika kuunganisha mafunzo ya vyuoni na mahitaji halisi ya soko la ajira kwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu, sekta binafsi na viwanda hatua itakayoongeza ujuzi unaohitajika katika mazingira ya kazi.
“Nikipongeze Chuo cha VETA Furahika kwa juhudi mnazofanya kutoa ujuzi kwa vijana wetu, lakini pia Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Bakari Shingo nimeambiwa hapa unasomesha wanafunzi 220 ambao wengine wamehitimu leo, haya ni mafanikio makubwa yanayotokana na ushirikiano mzuri ulipo baina yenu na Serikali," ameongeza Naibu Waziri Wanu.
Amewataka wahitimu kutumia elimu na ujuzi walioupata kujenga ajira na fursa za maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu, ubunifu, uzalendo na ujasiriamali katika kufanikisha malengo yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Bakari Shingo amesema mpaka sasa ameshafadhili wanafunzi 220 katika Chuo hicho akitumia utaratibu wa kutangaza fursa hizo kupitia gari la matangazo ili kutoa nafasi kwa kila kijana anayehitaji kupata ujuzi.
Mkuu wa Chuo Dkt. David Cleopa Msuya amesema kuwa Chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 460 na kinatoa kozi mbalimbali za ufundi ikiwemo Usimamizi wa hoteli, Kompyuta, Umeme, Urembo, Ushonaji, Utalii na Uondoshaji mizigo bandarini (Clearing and Forwarding).











No comments:
Post a Comment