
Mkaguzi wa Polisi katika Kata ya Tabata, Mkoani Dar es Salaam Mkaguzi wa Polisi (INSP) Judith Stesheni, ameendelea na kampeni yake ya kutoa elimu kwa jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya usalama mahala pakazi.
Katika mafunzo hayo Mkaguzi huyo amefika katika kituo cha uuzaji mafuta ambapo amekutana na wahusika wa biashara hiyo na kuwahimiza kuzingatia usalama wao pamoja na wateja wao pindi wanapobeba mafuta katika vyombo visivyo salama.
Amebainisha kiwa wauzaji hao, wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo katika uuzaji na usafirishaji wa mafuta ambapo ameeleza kuwa mafuta yanapaswa kubebwa na kuhifadhiwa katika vifaa maalum vilivyoruhusiwa na vinavyokidhi viwango vya ubora na usalama.
Aidha, amewataka kuacha mara moja tabia ya kubeba mafuta yenye viashiria vya milipuko katika vidumu visivyo salama, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa watu na mali.
Sambamba na hilo, amewahimiza wananchi na wafanyabiashara kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuimarisha ulinzi na usalama katika Kata ya Tabata.

No comments:
Post a Comment