MOI YAANZISHA HUDUMA 9 MPYA ZA KIBOBEZI, IKIWEMO UPASUAJI KWA AKILI UNDE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 2, 2026

MOI YAANZISHA HUDUMA 9 MPYA ZA KIBOBEZI, IKIWEMO UPASUAJI KWA AKILI UNDE


Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) imeanzisha huduma mpya tisa za kibobezi, ikiwemo upasuaji wa ubongo kwa kutumia teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence), hatua inayolenga kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo Machi 2, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa MOI, Dk. Mpoki Ulisubisya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk. Ulisubisya ametaja huduma nyingine zilizoanzishwa kuwa ni upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu (minimally invasive spine surgery), huduma ya kuchukua sampuli za vipimo kwa njia ya matundu, na huduma ya kuweka tiba ya simenti maalum katika pingili za mgongo zilizovunjika.

“MOI tumeanzisha huduma ya tiba ya maumivu, upasuaji rekebishi wa viungo vilivyopooza, upasuaji wa uvimbe wa ubongo kwa kutumia teknolojia ya fluorescein, pamoja na kuanza kwa wodi mpya za kisasa za Premier kwa wagonjwa maalum na wa kimataifa,” amesema.

Kutokana na upanuzi huo wa huduma, idadi ya wagonjwa imeongezeka ambapo kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana, MOI ilihudumia jumla ya wagonjwa 176,987.

Kwa mujibu wa Dk. Ulisubisya, taasisi hiyo imeendelea kutoa huduma za kibingwa bobezi na kupunguza rufaa za nje ya nchi, ikiwemo upasuaji na uchunguzi wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu, pamoja na upasuaji wa marudio wa nyonga na magoti.

Huduma nyingine ni matibabu ya kiharusi kupitia mishipa mikubwa ya damu, upasuaji wa kunyoosha mgongo uliopinda, kuondoa uvimbe wa ubongo kupitia tundu la pua, na matibabu ya maumivu sugu ya mgongo.

Amesema MOI pia inaendelea kuhudumia wagonjwa wa kimataifa kutoka mataifa ya Congo, Comoro, Uganda, South Sudan, Burundi na nchi nyingine nje ya Bara la Afrika.

Katika mwaka wa fedha 2025/2026, MOI imeendelea kutekeleza agizo la Serikali la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi kupitia huduma za tiba mkoba katika hospitali za Nyangao (Lindi), St. Benedict Ndanda, Nkinga (Tabora), Rufaa ya Kanda Chato, na Tosamaganga (Iringa).
Huduma hizo pia zimeanza kupatikana katika Hospitali ya Mwalimu Nyerere (Musoma) na ALMC (Arusha).

Dk. Ulisubisya amesema MOI imejipanga kuendelea kuboresha huduma ili kufikia viwango vya kimataifa na kupata ithibati ya kimataifa.

Aidha, taasisi hiyo inatarajia kuanza ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao katika kiwanja chake chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji jijini Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa hatua ya kusogeza baadhi ya huduma kutoka Upanga kwenda jengo jipya itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, huku taasisi ikiendelea kuanzisha huduma mpya za kibingwa ambazo hazipatikani nchini.

No comments:

Post a Comment