Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kufikisha umeme katika vijiji pamoja na pembezoni mwa mji hali iliyochochea kuongezeka kwa uwekezaji maeneo ya vijijini.
Mhe. Mtanda mesema hayo leo Aprili 16, 2026 Ofisini kwake alipokutana na Bodi, Menejimenti ya REA pamoja na Wabia wa Maendeleo, wanaoshirikiana na Wakala huo kwenye utekelezaji wa miradi yao Nchini.
“Nishati ya Umeme ni Nishati Muhimu, uwekezaji kwenye Kilimo na Mifugo hauwezi kufanyika kama hakuna Umeme. Ninao Wanawake wawili ambao wana miradi wa kufuga kuku zaidi ya 30,000 kila mmoja. Bila ya Nishati ya Umeme mradi wao hauwezi kuwa bora na endelevu.
Uwepo wa umeme vijijini umechochea miradi mbalimbali kuibuliwa na kutekelezwa maeneo ya vijijini hali inayochochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa pamoja na mtu mmoja mmoja,” amesema Mhe. Mtanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA Mhandisi Jones Olotu, amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwapa fursa Wabia hao wa Maendeleo kutembelea na kujionea miradi inayotekelezwa na Wakala.
“Wabia hawa tumekuwa tukishirikiana nao kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali na hivyo leo wameweza kuja kujionea utekelezwaji wa miradi ya nishati vijijini,” amesema Mhandisi Olotu.
Faraja Nyoni ambaye ni Msimamizi wa shamba la Mwasonge, ambao pamoja na shughuli zingine, wanafuga kuku zaidi ya 30,000, amesema kuwa uwepo wa umeme umeweza kuwasaidia kutekeleza mradi huo kisasa na kupunguza gharama za uendeshaji.
Amesema awali walikuwa wakitumia zaidi ya shilingi milioni nne kwa ajili ya kuweka mafuta ya jenereta kuendeshea shughuli zao katika mradi huo lakini kwa sasa wanatumia shilingi milioni moja tuu.
Naye Mhandisi Wiston Nnko ambaye ni mhandisi wa mradi wa kukausha dagaa kwa kutumia umeme jua kutoka kampuni ya Millenium Engineers ameshukuru na kuipongeza REA kwa kuweza kuwawezesha wawekezaji mbalimbali wakiwamo wao hali iliyowawezesha kuongeza thamani ya soko la dagaa.



















No comments:
Post a Comment