
Na Shua Ndereka, OKULY BLOG Morogoro
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawatafuta ndugu wa mtu mmoja aliyefariki dunia ghafla baada ya kushuka kwenye gari la abiria katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani Msamvu.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, inaeleza kuwa, tukio hilo limetokea Machi 22, 2026 jioni katika kituo hicho cha mabasi, kilichopo Kata ya Mafisa, Manispaa ya Morogoro.
Aidha, marehemu alitambulika kwa majina ya Reuben Masimba Chedego mwenye umri wa miaka70, mkulima na mkazi wa Chalinze, ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuwa alikufa ghafla muda mfupi baada ya kushuka kwenye gari la abiria akitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro.
“Alipokwenda kupata haja ndogo aliishiwa nguvu, akadondoka na kisha kupelekwa hospitali ya mkoa kwa huduma, ambapo ilithibitika kuwa tayari alikuwa amefariki, kabla ya kufikishwa hospitalini,” amesema Kamanda Mkama.
Kamanda Mkama amesema kuwa, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi na utambuzi kutoka kwa ndugu zake.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi linachunguza taarifa ya kifo cha mtoto wa miaka 12 aliyefariki kwa kujinyonga baada ya kukemewa na wazazi wake kuachana na tabia ya udokozi.
Kifo cha mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Rajab Ally Mohammed kimebainika mapema Machi 23, 2026 katika Kata ya Italagwe, Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, ambapo alijinyonga nyuma ya nyumba yao ya kuishi.
Aidha, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo alikemewa na wazazi wake Machi 22, 2026 kuacha vitendo vya udokozi baada ya kukamatwa na wenzake wawili wakiwa wameiba mahindi mabichi.
“Kitendo cha kukemewa kilimjaza hasira na kuamua kujiua kwa kutumia mkanda wa suruali yake,” amesema Kamanda Mkama.
Kamanda Mkama ametoa wito, kwa watoto wote kusikiliza vyema mafundisho ya wazazi, walimu na viongozi wa kijamii ili wakue katika maadili mazuri na kuepuka mwenendo mbaya wa kujichukulia sheria mkononi, kwa hasira kiasi cha kujifanyia ukatili unaosababisha kifo.

No comments:
Post a Comment