
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Palamagamba Kabudi, amefanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Robert Oliphant.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini London, Uingereza, pembezoni mwa Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Machi 8, 2026, ambapo viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Canada pamoja na kuendeleza uhusiano wao ndani ya Jumuiya ya Madola kwa kuzingatia misingi na tunu za jumuiya hiyo katika kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja.
Viongozi hao wamebainisha kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Canada umejengwa juu ya msingi wa urafiki wa kihistoria, ushirikiano wa kiuchumi pamoja na uanachama wao ndani ya Jumuiya ya Madola, hali inayofungua fursa zaidi za kupanua ushirikiano katika nyanja za biashara, uwekezaji na kubadilishana uzoefu katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Aidha, viongozi hao wameangazia mchango wa diaspora wa Tanzania na Canada katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi zao.
Walieleza kuwa kupitia uhusiano wao ndani ya Jumuiya ya Madola, diaspora imeendelea kuwa kiungo muhimu kinachoimarisha uhusiano wa watu kwa watu na kufungua fursa zaidi za ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Katika mazungumzo hayo, Prof. Kabudi aliambatana na Mshauri wa Rais katika Masuala ya Diplomasia, Balozi Lazaro Nyalandu; Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki; pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda.










No comments:
Post a Comment