SERIKALI KUANZISHA MFUMO WA KIDIJITALI (PORTAL) KUHIFADHI NA KUSAMBAZA TAFITI NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 23, 2026

SERIKALI KUANZISHA MFUMO WA KIDIJITALI (PORTAL) KUHIFADHI NA KUSAMBAZA TAFITI NCHINI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali imepanga kuanzisha mfumo wa kidijitali (portal) wa kuhifadhi na kusambaza tafiti zote zinazofanyika nchini, hatua inayolenga kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika ipasavyo katika kufanya maamuzi ya kisera na kupanga maendeleo ya taifa.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, wakati akifungua mkutano wa kitaifa unaowakutanisha taasisi za utafiti, uliofanyika Machi 23, 2026 jijini Dodoma.

Dkt. Kida amesema mfumo huo utasaidia kuimarisha upatikanaji wa taarifa za tafiti, kuongeza uwazi, pamoja na kuwezesha wadau mbalimbali kuzitumia tafiti hizo katika kubuni sera na mipango yenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Amesema Tanzania ipo katika hatua muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kujenga uchumi wa trilioni moja na kuboresha ustawi wa wananchi.

Aidha, dira hiyo inalenga kutokomeza umasikini uliokithiri, kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, pamoja na vifo vya watoto wachanga ifikapo mwaka 2050.

“Tutahakikisha kuwa hakuna Mtanzania atakayebaki katika umasikini uliokithiri, huku tukiboresha huduma muhimu za kijamii kama afya na elimu,” amesema Dkt. Kida.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa dira hiyo utaendeshwa kupitia mipango ya muda mrefu itakayogawanywa katika vipindi vya miaka mitano mitano, huku kila mwaka ukiwa na mpango mahsusi wa utekelezaji wenye vipaumbele vya kitaifa.

Dkt. Kida amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Mipango itaendelea kuwa mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya uchumi na maendeleo, na kusimamia pamoja na kuratibu utekelezaji wa mipango hiyo.

Akizungumzia umuhimu wa tafiti, amesema tafiti za kiuchumi na kijamii ni nyenzo muhimu katika kubuni sera bora, kuboresha utekelezaji wa mipango, na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

“Ni muhimu kuwa na mwongozo madhubuti wa tafiti unaozingatia vipaumbele vya taifa ili kuhakikisha matokeo yake yanatatua changamoto halisi za wananchi,” amesisitiza.

Amebainisha kuwa tafiti hizo zitachangia maendeleo ya uchumi, jamii na mazingira, hususan katika kukabiliana na changamoto zinazoibuka ikiwemo ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya tabianchi.

Awali akizungumza,Naibu Katibu Mtendaji - Mipango ya Kitaifa, Dkt. Mursali Milanzi amebainisha kuwa Tume ya Taifa ya Mipango ina jukumu la kusimamia na kushauri masuala ya uchumi, ikijumuisha kuchambua hali ya mfumuko wa bei, uwiano wa mapato na matumizi ya Serikali, pamoja na kuhakikisha uchumi unakuwa na utulivu na ukuaji endelevu. Pia ameongeza kuwa Tume inaratibu na kuongoza mipango ya kitaifa, kisekta na kitaasisi ili iendane na Dira ya Taifa na utekelezwe kupitia mipango ya muda mrefu, wa kati na wa mwaka.

‎Aidha, amesema kuwa Tume hufanya tathmini ya sera kuhakikisha zinatoa matokeo yanayotarajiwa na kutoa ushauri wa kuboresha pale inapobidi. Pia inahakikisha mipango ya sekta mbalimbali inafungamana na malengo ya kitaifa ili kuepuka migongano ya utekelezaji, huku ikiendelea kuimarisha taaluma ya mipango kupitia majukwaa kama Mkutano wa Wapangaji

Mkutano huo wa siku mbili unalenga kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za utafiti, ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika nchini zinaendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Kwa ujumla, Tanzania inaendelea kujipanga kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii, yakilenga kukuza uchumi shindani na jumuishi, kuongeza ajira na tija, pamoja na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment