
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya, amewataka watumishi wa umma kuweka kipaumbele katika afya ya akili, kuepuka msongo wa mawazo, na kujijengea uwezo wa kiuchumi kupitia ujasiriamali ili kuwa na maisha bora wakati wa utumishi na baada ya kustaafu.
Akizungumza Machi 31, 2026 jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Mhe. Kasekenya alisema mada zinazohusu afya ya akili, udhibiti wa msongo wa mawazo, ujasiriamali na ajira ni muhimu kwa watumishi kutokana na changamoto za mazingira ya kazi wanazokutana nazo kila siku.
“Mada hizi zinalenga kuwasaidia watumishi kuwekeza kupitia ujasiriamali na kujiandaa kwa maisha ya baada ya kustaafu,” alisema Mhe. Kasekenya.
Alieleza kuwa wajumbe wa baraza wana jukumu la kuwakilisha watumishi wenzao kwa ufanisi na kuhakikisha wanarejesha maazimio ya vikao ili kuboresha utendaji kazi na kufikia malengo ya Wizara.
Aidha, Mhe. Kasekenya alibainisha kuwa baraza la mwaka huu limefanyika kwa vikao viwili vikijikita katika tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na majadiliano ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, yakilenga kuimarisha utendaji na maslahi ya watumishi.
Pia aliwasisitiza watumishi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi, huku wakiepuka vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi, ili kufanikisha azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Awali akizungumza, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, alisema mkutano huo umetoa fursa ya kujadili hoja mbalimbali za matumizi, kutoa ufumbuzi na kuweka mikakati mipya ya kuboresha ustawi wa watumishi.
Aliongeza kuwa mada za uwekezaji na ujasiriamali zimewasaidia watumishi kuona fursa za kuongeza kipato hata kwa wenye mishahara midogo, huku wakijijengea msingi imara wa kifedha.
Kwa upande mwingine, baraza lilijadili pia umuhimu wa lishe bora na afya ya mwili, pamoja na afya ya akili ili kuongeza ufanisi kazini.
Vilevile, wajumbe walipitia mikakati ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ikiwemo barabara na madaraja, pamoja na namna ya kushirikisha sekta binafsi na kuimarisha udhibiti wa mizani ili kulinda ubora wa barabara.
Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi ulianza Machi 30, 2026 na kuhitimishwa Machi 31, 2026 jijini Dodoma.


No comments:
Post a Comment