Na. Saidina Msangi, WF, Dar es Salaam.
Serikali imewahakikishia wamiliki na wadau wa viwanda nchini kuwa inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara, huku ikibainisha kuwa mapendekezo yaliyowasilishwa na wadau hao yanafanyiwa kazi kwa kina kuelekea kipindi cha Bunge la Bajeti.
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), iliyowakutanisha viongozi wa Serikali na wadau wa viwanda kwa lengo la kutathmini, kuoanisha mikakati, na kutatua changamoto zinazozuia kasi ya ukuaji wa sekta hiyo, iliyofanyika xkatika ukumbi wa hotel ya Four Point, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya viwanda katika kukuza uchumi wa Taifa na kutengeneza ajira hivyo Serikali imepokea mapendekezo yao na itayafanyia kazi kwa umakini mkubwa.
‘’Serikali imekuwa ikisikiliza maoni ya wadau ambapo zaidi ya asilimia 60 ya mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa viwanda mwaka jana yalifanyiwa kazi na Serikali katika mwaka wa fedha 2025/2026 hali inayodhihirisha kuwa sekta binafsi ni mshauri mkuu na wa kuaminika katika uendeshaji wa viwanda nchini,’’ alisema Mhe. Luswetula.
Alisema kuwa Wizara ya Fedha imepokea mapendekezo mapya yanayolenga zaidi kodi za bidhaa na gharama za uzalishaji na kueleza kuwa yatafanyiwa kazi ambapo baadhi ya kodi zinatarajiwa kupunguzwa au kuondolewa kabisa ili kumpa nafuu mfanyabiashara na mwananchi wa kawaida.
Aliongeza kuwa majibu ya jumla yatakayotolewa baada ya mchakato wa bajeti yataakisi mahitaji ya soko na kusaidia viwanda vya ndani kuwa na ushindani zaidi.
Alifafanua kuwa Dira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
"Serikali inawathamini sana, tumepokea mapendekezo yenu na tunaenda kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa lengo ni kutengeneza kitu bora kitakachojenga uchumi wa nchi hii kwa ajili ya wenye viwanda na wananchi wote," alisema Mhe. Luswetula.
Pia aliwapongeza wadau kwa ushirikiano wao na kubainisha kuwa Serikali itaendelea kuwaita viongozi wa sekta hiyo kwa majadiliano zaidi ili kuhakikisha kila hatua katika maboresho ya sera za kodi inalenga kukuza viwanda vya ndani.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, alieleza kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na CTI ili kuhakikisha sera na mipango inayotekelezwa inatoa matokeo chanya katika ustahimilivu wa sekta ya viwanda na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Alisema dhamira ya Serikali ni kuendeleza viwanda kama muhimili mkuu wa mabadiliko ya kiuchumi na injini ya kutengeneza ajira, kuongeza thamani ya rasilimali ghafi, na kukuza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, hivyo itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa nishati ya uhakika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Bw. Leodgar Tenga, alisema kuwa mazungumzo yalilenga kuimarisha sekta ya viwanda ili viweze kufanya vizuri kuinua uchumi, kuwezesha upatikaji wa ajira pamoja na kuwezesha utengenezaji wa bidhaa ambazo zinaweza kushindana katika soko.








No comments:
Post a Comment