WADAU WA MAJI NA MADINI KUKUTANA MWANZA KUJADILI USALAMA WA MABWAWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 31, 2026

WADAU WA MAJI NA MADINI KUKUTANA MWANZA KUJADILI USALAMA WA MABWAWA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali kupitia Wizara ya Maji imetangaza kufanyika kwa Mkutano wa Mwaka wa Usalama wa Mabwawa utakaofanyika jijini Mwanza Oktoba 21–23, 2026, ukilenga kuimarisha usalama wa miundombinu ya mabwawa ya maji na tope sumu huku wataalam, wadau na wamiliki wa mabwawa wakihimizwa kushiriki.

Akizungumza na waandishi wa habari Machi 31, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Robert Sunday, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema mkutano huo unaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji, Taasisi ya Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) na Kampuni ya City Engineering, ukiwa ni mwendelezo wa juhudi za Serikali kuhakikisha mabwawa yanakuwa salama kwa matumizi ya kijamii na kiuchumi.

Sunday alieleza kuwa Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 toleo la 2025 inaweka mkazo katika uendelezaji wa rasilimali za maji, ikiwemo ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua, kukabiliana na mafuriko pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wa kiangazi.

Aliongeza kuwa ukuaji wa sekta ya madini umeongeza uhitaji wa mabwawa ya kuhifadhi tope sumu (TSF), ambayo licha ya umuhimu wake, yanaweza kuwa hatari kwa mazingira na vyanzo vya maji iwapo hayatadhibitiwa ipasavyo.

Kwa mujibu wa Sunday, Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji ina jukumu la kusimamia usalama wa mabwawa hayo kwa kuzingatia sheria na kanuni, pamoja na kuwajengea uwezo wadau kupitia mafunzo na mikutano ya kitaalamu.

Amesema kwa miaka minne mfululizo, Wizara imekuwa ikiandaa mikutano na mafunzo hayo, ambapo mwaka 2025 zaidi ya washiriki 200 walinufaika na mafunzo ya kukabiliana na majanga ya mabwawa, yakishirikisha wataalam kutoka Afrika Kusini.

Aidha, Serikali inaendelea na mchakato wa kujiunga na Taasisi ya Kimataifa ya Mabwawa Makubwa (ICOLD) ili kuongeza uwezo wa kitaalamu na usimamizi wa mabwawa nchini.

Katika mkutano wa mwaka huu, mafunzo yatazingatia mada ya “Usalama wa Miundombinu ya Mabwawa,” yakihusisha hatua zote kuanzia usanifu, uendeshaji hadi ufungaji, huku yakilenga kuongeza ujuzi kwa wataalam na wadau wa sekta hiyo.

Sunday ametoa wito kwa watunga sera, wataalam, wamiliki wa mabwawa na wadau wengine kujisajili kushiriki mkutano huo kupitia tovuti rasmi ya mkutano huo.

Ameishukuru Chemba ya Migodi Tanzania na Kampuni ya City Engineering kwa ushirikiano wao unaochangia kuimarisha usalama wa mabwawa na uhifadhi wa rasilimali za maji nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania, Bw. Benjamini Mchwampaka, ameeleza kuwa mikutano na mafunzo ya kila mwaka yamekuwa fursa muhimu kwa wadau wa sekta ya maji na madini kuungana, kubadilishana ujuzi na kukabiliana na changamoto zinazohusiana na usalama wa mabwawa. Amesistiza kuwa ushirikiano huu unasaidia kulinda maisha ya watu, mali zao, na mazingira, huku wakishirikiana na wataalamu wa ndani na wa kimataifa.

‎kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa City Engineering, Bw. Anael Macha, ameongeza kuwa mkutano huo ni nafasi ya moja kwa moja kwa wadau wa sekta ya madini na maji kujadili, kuwasilisha bidhaa na huduma zao, na kupata uungwaji mkono wa kiufundi na kifedha.

‎Mafunzo haya yanakuja sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025–2050, ikizingatia uadilifu wa mazingira, usalama wa mabwawa, na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na tope sumu, na kuimarisha jitihada za Tanzania katika kuhakikisha mabwawa yote yanaendelea kuwa salama.

No comments:

Post a Comment