WANAWAKE -MSINGI WA USALAMA WA RASILIMALI MAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, March 8, 2026

WANAWAKE -MSINGI WA USALAMA WA RASILIMALI MAJI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri akikagua ujenzi wa tanki la Maji la mradi wa miji 28 Mafinga,Njombe.

Na Annamaria Bonda


Mjukuu wangu, unapomaliza kuchota maji hakikisha unafunga bomba la maji vizuri ili maji yasipotee. Maji hapa kwetu yana thamani kubwa sana kuliko chochote kile”, Bibi Fatuma Hanzuruni (62) mkazi wa pembezoni kabisa mwa Tanzania, mji wa Ujiji, mkoa wa Kigoma anasema.* 

Maneno hayo yanasadifu uhalisia wa maisha ya jamii, hususan kwa wanawake wengi wa Tanzania kwa miaka ya nyuma. Alfajiri kabla ya jua kuchomoza, mazingira ya ukungu na umande, wanawake na watoto wa kike wanabeba ndoo za maji na mitungi vichwani, wakitembea umbali mrefu kuelekea ziwani, visimani, mito na mabwawani kutafuta maji kwa maumizi ya nyumbani, ikiwamo kunywa na kutunza usafi katika familia zao. 

Changamoto zilikuwa nyingi ikiwamo umbali mrefu wa kutafuta vyanzo vya maji ili kupata maji ingawa sio salama kwa ajili ya matumizi mbalimbali, jukumu hilo ikiambatana na hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali, migogoro ya kifamilia, uchumi duni kwa kutumia muda mrefu kutafuta maji na kukosa fursa ya elimu kama inavyotakiwa kwa watoto au kushiriki katika maamuzi muhimu ya kijamii. Wakati mwingine safari hizo zikigharimu afya zao, ulemavu au hata maisha. 

Hata hivyo, hivi leo mapinduzi makubwa yamefanyika, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa katika jamii ya Tanzania katika maeneo tofauti. 

Kupitia juhudi za Serikali katika kuimarisha Sekta ya Maji, miradi mingi ya usambazaji maji imejengwa na kupanuliwa kote nchini. Huduma ya majisafi na salama sasa inapatikana kwa urahisi zaidi, ndani ya umbali usiozidi mita 60 katika makazi ya wananchi.

Wanawake hawabebi tena ndoo kichwani kwa masafa marefu wala kutumia muda mwingi kutafuta maji; badala yake, muda wao sasa unaelekezwa katika shughuli za uzalishaji kama kilimo, biashara na malezi bora ya familia, hivyo kuinua jamii kiuchumi. 

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani nchini Tanzania inayoambatana na kaulimbiu ya “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050,”, mafanikio katika Sekta ya Maji ni ushuhuda wa hatua muhimu kuelekea usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi. 

Serikali ya Awamu ya Sita imeendeleza azma ya “kumtua mama ndoo ya maji kichwani.” Hatua zilizochukuliwa kufanikisha azma hiyo imeongeza upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 79.9 hadi asilimia 85.2 huku mijini upatikanaji umeongezeka kutoka asilimia 84 hadi 92.5 katika kipindi hadi mwezi Desemba 2025. Takwimu hizi zinazidi kuimarishwa kwa kazi mbalimbali za miradi ya maji inayoendelea kujengwa na serikali.

Kwa ujumla, miradi 1,965 ya maji vijijini imekamilika, ikihudumia vijiji 5,521 na kuongeza idadi ya vijiji vyenye huduma ya maji kufika 10,779 kati ya 12,333 vilivyopo nchini. Aidha, miradi 366 ya maji mijini imekamilika, ikihudumia zaidi ya wananchi milioni 6.2. 

Miongoni mwa miradi ya kimkakati inayoendelea na ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni Mradi wa Bwawa la maji la Kidunda mkoani Morogoro, Mradi wa Maji wa Kiwira mkoani Mbeya, Mradi wa Miji 28 unaotekelezwa katika mikoa mbalimbali, Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa Simiyu na unatumia chanzo cha maji cha ziwa Victoria, pamoja na baadhi ya miradi iliyokamilika kama Same–Mwanga–Korogwe, utoaji maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda Mugango-Kiabakari-Butiama, Tinde-Shelui, Nzega-Igunga-Tabora na Butimba- Mwanza. Miradi hii ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji ili kuhakikisha huduma ya maji endelevu kwa Watanzania wote nchini. Mpango huu unahusisha kutoa maji katika mito mikubwa na maziwa na kupeleka katika maeneo yanye upungufu wa vyanzo vya maji. 

Ni muhimu kuelewa kuwa Wizara ya Maji imebeba jukumu la kufikisha huduma hii kwa wananchi ikiwa maji si tu hitaji la kila siku bali ni uti wa mgongo wa maendeleo ya uchumi wa taifa. Katika jamii nyingi, mwanamke ndiye mhimili wa matumizi, uhifadhi na usimamizi wa maji. Hivyo, kumwezesha mwanamke kuwa na uwezo wa kusimamia vyanzo vya maji ni hatua ya kuimarisha usalama wa rasilimali maji. 

Aidha, kuwapa wanawake na wasichana elimu na kuwashirikisha kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira , vyanzo vya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni jambo la muhimu kwa maendeleo ya vizazi kwa sasa na wakati ujao. 

Hii ina maana usimamizi madhubuti wa rasilimali za maji ni nguzo ya maendeleo endelevu na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo. Hivyo inahitaji kuongeza uelewa wa jamii, kuhamasisha matumizi bora ya maji, na kuimarisha mikakati ya uhifadhi wa mazingira. 

Akitoa hotuba wakati akifungua Bunge, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 14 Novemba 2025, alisisitiza kuwa:

“Mimi ni mama, na asilimia kubwa wanaoteseka juu ya adha ya maji ni akina mama. Sitaki kusikia wala kuona wanawake wa nchi hii wanateseka na adha ya maji.

“Naomba Mungu Awamu ya Sita isipimwe tu kwa vitu vitakavyoachwa, bali pia kwa tabasamu la utu litakaloachwa katika nyuso za Watanzania.”

Maneno haya yanathibitisha dhamira ya Serikali kuchukua hatua ya lazima kumaliza kero ya upatikanaji wa maji kwa
wananchi wake.

Hakika, miongoni mwa vitu vinavyoleta tabasamu hilo kwa Mtanzania ni uhakika wa upatikanaji wa huduma ya uhakika ya majisafi na salama kwa kila mwananchi, mjini na vijijini. 

Ili kuweza kutimiza lengo hilo wanawake na wasichana ni walinzi, wahamasishaji na viongozi katika kulinda na kutunza rasilimali maji. Uwepo wao katika sekta hii si chaguo, bali ni msingi wa mafanikio yake. 

“Jukumu langu la msingi ni kuhakikisha huduma ya maji inafika kwa kila mwananchi, jukumu ambalo nitalifanya kwa weledi wangu wote” - Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri. 

Maneno haya yanachora mstari kuonesha nafasi ya mwanamke kufikia kilele cha mafanikio ya Sekta ya Maji katika taifa la Tanzania.

Kukosekana kwa huduma ya maji hurudisha kumbukumbu za makovu ya kale, hali ambayo taifa halipaswi kuruhusu ijirudie. Kwa kutambua hilo Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kupitia mikakati mbalimbali kuboresha huduma ya maji mijini na vijijini sasa na baadaye. 

Jitihada hizi zinaipa nguvu safari ya maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania kwa kuwa sekta zote zinategemea maji ili ziweze kupiga kwa hatua. Maji ni chachu katika kuleta mafanikio kwa sekta nyingine. Hii inadhihirisha kuwa maji sio huduma pekee bali ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi.

No comments:

Post a Comment