e-GA YAIMARISHA TEHAMA SERIKALINI: TAASISI 571 ZAFIKIWA NA MABORESHO YA USALAMA NA MIFUMO YA KIDIJITALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 17, 2026

e-GA YAIMARISHA TEHAMA SERIKALINI: TAASISI 571 ZAFIKIWA NA MABORESHO YA USALAMA NA MIFUMO YA KIDIJITALI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imepanga kuimarisha usalama wa mifumo ya TEHAMA, kuongeza ufanisi wa huduma za kidijitali na kuunganisha taasisi za umma katika mfumo mmoja jumuishi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hayo yameelezwa Aprili 17, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani J. Kikwete, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Waziri Kikwete amesema katika mwaka huo wa fedha e-GA itafanya tathmini na usimamizi wa usalama wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA katika taasisi 571 za umma, hatua inayolenga kuhakikisha mifumo hiyo inafanya kazi kwa ufanisi na usalama wakati wote.

Aidha, Serikali itaimarisha mifumo jumuishi ya TEHAMA pamoja na mifumo ya kisekta na kitaasisi ili kuhakikisha huduma za kidijitali zinaboreshwa na kuondoa urudufu wa mifumo isiyohitajika serikalini.

Katika hatua nyingine, e-GA itafanya uchambuzi, usanifu na ujenzi wa mifumo mipya ya kisekta kwa taasisi mbalimbali ili kupunguza wingi wa mifumo na kuongeza ushirikiano wa kiutendaji kati ya taasisi za umma.

Serikali pia itaunganisha mifumo ya taasisi zote kupitia Mfumo wa Serikali wa kubadilishana taarifa (GovESB), hatua inayolenga kurahisisha mawasiliano na ushirikiano wa kidijitali serikalini.

Vilevile, Mamlaka hiyo itaimarisha utafiti na ubunifu katika matumizi ya teknolojia mpya za TEHAMA ili kuibua huduma mpya kwa wananchi, sambamba na kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia zinazoendelea kujitokeza duniani.

Katika kuboresha huduma, Serikali itaongeza wigo wa mtandao wa mawasiliano wa serikali hadi kufikia wilaya zote nchini, pamoja na kuimarisha mifumo kama e-Office na huduma nyingine za kidijitali.

Aidha, e-GA itaendelea kusimamia miundombinu ya TEHAMA ikiwemo vituo vya kuhifadhi taarifa za serikali na mifumo ya kujikinga na majanga ya kidigitali.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Serikali pia itatoa mafunzo kwa watumishi wa umma na watumiaji wa mifumo ya TEHAMA ili kuhakikisha matumizi salama na yenye ufanisi wa teknolojia katika utumishi wa umma.

Hatua hizo zinalenga kuimarisha utawala bora wa kidijitali, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi wa huduma za serikali kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment