
Na Mwandishi Moshi, Kilimanjaro
Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) chini ya mradi wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) inalenga kuongeza mtandao wa barabara za lami Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro sambamba na kukarabati na kujenga mifereji ya maji ya mvua itakayosaidia kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kuondoa kero ya mafuriko.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum, Mratibu wa mradi wa TACTIC Manispaa ya Moshi Mhandisi Daniel Kileo ameishukuru serikali kwa kuleta mradi huo kwani utasaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi, biashara na kijamii, kupunguza foleni, kuongeza fursa za ajira, thamani ya ardhi kupanda, na kuongeza mapato ya halmashauri baada ya kukamilika.
"Mradi huu unakuja kama mkombozi kwenye Manispaa yetu, ujenzi wa barabara za lami Km 14 zitapendezesha mji pia ujenzi wa mfereji wa Kibong'oto Km 1.9 kata ya Kilimanjaro na ujenzi wa mfereji katika barabara ya Chuo cha Ushirika-Kizz Hotel-Moshi Pazuri Km 2.02 itasaidia kuondoa maji katika makazi ya watu", amesema.
Ameongeza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 na unatarajiwa kukamilika tarehe 24 Januari 2027 ambapo mpaka sasa umefikia asilimia 5 kwa gharama ya shilingi Bilioni 24.4 kupitia mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Aidha, amesema kuwa miongoni mwa barabara zitakazojengwa ni barabara ya Ruwaichi-Njoro Km 6.85 inayounganisha kata za Ng'ambo, Msaranga, Mji mpya na Njoro, barabara ya Pepsi Km 1.25 inayounganisha kata ya Kaloleni na Njoro, barabara ya Shirima Tunda-Magereza Km 5.089 inayounganisha kata ya Karanga na Shirima Tunda.
Kwa upande wake, Fundi Sanifu TARURA wilaya ya Moshi Bi. Joyce Kapelo amesema kuwa TARURA wilaya ya Moshi ina mtandao wa barabara za lami Km 105 kupitia mradi zitaongezeka Km 14 na kufikia Km 119 za lami, hivyo wanaishukuru serikali kwa mradi huo utakaosaidia kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi.
Naye, Diwani wa kata ya Shirima Tunda Mhe. Francis Shio ameishukuru serikali kwa ujenzi wa barabara ya Shirima Tunda-Magereza ambayo ni barabara kuu ya kuelekea Arusha ambapo kukamilika kwa barabara hiyo kutaongeza fursa za biashara na huduma za kijamii kufikika kwa urahisi. Pia amewaomba wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Bw. Mtui Jacob mkazi wa kata ya Ng'ambo ameeleza kuwa hapo awali kipindi cha mvua barabara zilikuwa hazipitiki zilikuwa na makorongo walikuwa wanatembea hadi Km 4 kufika mjini lakini barabara ikikamilika usafiri utakuwa karibu na kurahisisha kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.
Naye, Bi. Lucy Macha mkazi wa mtaa wa Msaranga ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo amesema lami ikiwekwa itawasaidia kupata wateja wengi na pia taa zikiwekwa watafanya biashara hadi usiku na kusaidia kuimarisha usalama katika maeneo yao.






No comments:
Post a Comment