NJE SPORTS YATOA MSAADA NA KUPELEKA TABASAMU KATIKA MAKAO YA WATOTO NJOMBE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 28, 2026

NJE SPORTS YATOA MSAADA NA KUPELEKA TABASAMU KATIKA MAKAO YA WATOTO NJOMBE


Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Timu ya Michezo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ‘Nje Sports’, imetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila na kuleta faraja kwa jamii.

Tukio hilo limefanyika Aprili 28, 2026, ambapo timu hiyo ilitembelea vituo viwili vinavyotoa huduma ya malezi na hifadhi kwa watoto (Makao ya Watoto) ambavyo ni Kituo cha Renato Grandi na Kituo cha Hospitali ya Ilembula, vilivyopo Wilayani Wanging'ombe mkoani humo.

Msaada uliokabidhiwa unajumuisha mahitaji muhimu ya kibinadamu yakiwemo chakula (sukari, mchele,maharagwe na mafuta ya kupikia) na vifaa vya usafi (sabuni, mafuta ya kupaka na nepi za watoto) ambayo yatasaidia kupunguza changamoto za uendeshaji wa vituo hivyo ambavyo vinalea watoto yatima na waliookolewa kutoka katika mazingira hatarishi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa Nje Sports, Bw. Ismail Abdallah, amewapongeza wanamichezo hao kwa moyo wa kujitolea na kuwasisitiza kuendelea kuwa kielelezo cha msaada kwa jamii. Aidha amewapongeza wasimamizi wa vituo hivyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwalea na kuwapa faraja watoto hao.

Kwa upande wao, wasimamizi wa Kituo cha Renato Grandi na Uongozi wa Hospitali ya Ilembula wameishukuru Nje Sports kwa upendo waliouonesha, wakibainisha kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya maisha kwa watoto wanaoishi katika makao hayo.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe, Bw. Barnabas Sichone, amepongeza hatua hiyo akisema imeacha alama chanya wilayani humo. Amebainisha kuwa kitendo cha Watumishi wa umma kujitolea kusaidia wenye uhitaji ni ishara ya ukomavu wa kiutumishi, uzalendo na utu wa kweli.

Miongoni mwa Viongozi waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ilembula, Muuguzi Mkuu, Katibu wa Afya wa Hospitali hiyo pamoja na Afisa Mtendaji wa Kata ya Ilembula.







No comments:

Post a Comment