
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, imeeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27 itaendelea kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha utoaji wa huduma kwa taasisi za umma na wananchi kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa Aprili 17, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Waziri Kikwete amesema moja ya vipaumbele vikuu ni kuimarisha uwajibikaji wa viongozi wa umma kupitia elimu ya maadili na matumizi ya mifumo ya kisasa ya TEHAMA, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza mianya ya uvunjifu wa maadili.
Amefafanua kuwa Ofisi hiyo itaendelea kupokea na kuhakiki matamko ya rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398, pamoja na kuchunguza tuhuma za uvunjifu wa maadili na kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi.
Aidha, Sekretarieti hiyo itaratibu na kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, sambamba na kutoa elimu kwa viongozi na wananchi kuhusu Sheria ya Maadili na Hati ya Ahadi ya Uadilifu.
Katika kuimarisha uadilifu kuanzia ngazi za chini, Serikali pia imepanga kuanzisha na kuendeleza klabu za maadili katika shule na vyuo mbalimbali nchini, ili kujenga kizazi chenye maadili na uwajibikaji.
Kwa upande wa miundombinu, Ofisi hiyo itaendelea na ujenzi wa ofisi kanda mbalimbali ikiwemo Kanda ya Ziwa (Mwanza), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Mashariki (Morogoro) pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Jengo la Kanda ya Kaskazini (Arusha).
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Ofisi hiyo imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 18.07, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 15.07 kimepangwa kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Serikali imesema hatua hizo ni sehemu ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma, sambamba na kuendeleza jitihada za kujenga utawala bora nchini.

No comments:
Post a Comment