SEKRETARIETI YA AJIRA YAAHIDI MAPINDUZI MAKUBWA YA USAILI NA AJIRA SERIKALINI 2026/27 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 17, 2026

SEKRETARIETI YA AJIRA YAAHIDI MAPINDUZI MAKUBWA YA USAILI NA AJIRA SERIKALINI 2026/27



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, imetangaza mpango mpana wa kuboresha mifumo ya ajira serikalini kwa mwaka wa fedha 2026/27, ukiwemo uimarishaji wa usaili, matumizi ya TEHAMA na kuongeza uwazi katika mchakato wa ajira.

Hayo yameelezwa Aprili 17, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani J. Kikwete, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Katika mpango huo, Sekretarieti ya Ajira imepanga kufanya jumla ya saili 22 kwa taasisi mbalimbali za umma, huku pia ikisimamia usaili 14 uliokasimiwa kwa vyuo vikuu vya umma na usaili 10 kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Aidha, Serikali imesema itaendesha usaili wa kuandika kwa kada 600 pamoja na usaili wa vitendo kwa kada 250, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na haki katika mchakato wa ajira serikalini.

Katika kuimarisha mifumo ya kidijitali, Sekretarieti hiyo itakusanya na kuhifadhi zaidi ya maswali 130,000 ya usaili kwenye kanzidata maalum, huku maswali 50,000 yakihuishwa kutoka kwenye mfumo huo kwa matumizi ya baadaye.

Vilevile, Serikali itaendelea na uhakiki wa vyeti na nyaraka za waombaji kazi ili kubaini sifa halisi za waombaji na kudhibiti udanganyifu katika ajira za umma.

Kwa upande wa mafunzo, waajiri 100 watapatiwa elimu kuhusu Mfumo wa Kupima Haiba na Tabia (Psychometric Test System), sambamba na mafunzo kwa watumishi 146 wa Sekretarieti ya Ajira kuhusu mifumo mipya ya TEHAMA.

Serikali pia imepanga kuboresha Mfumo wa Ajira Portal kwa kuunganisha na mifumo ya taasisi mbalimbali ikiwemo TCU, Mabaraza ya Afya na mfumo wa walemavu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na mfumo wa taarifa za wakimbizi.

Katika kuongeza uelewa kwa wananchi, kampeni tano za uhamasishaji kuhusu mifumo ya TEHAMA zitafanyika, pamoja na kampeni 20 zinazohusu taratibu za ajira nchini.

Aidha, Sekretarieti hiyo imepanga kuanzisha ofisi za kanda saba nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Sekretarieti ya Ajira imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 19.29, ambapo asilimia 92.7 ni kwa matumizi ya kawaida na asilimia 7.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Hatua hizo zinalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika mchakato wa ajira serikalini, sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utumishi wa umma.

No comments:

Post a Comment