TUME YA UTUMISHI WA UMMA KUIMARISHA UKAGUZI NA MFUMO WA RUFANI KUPITIA TEHAMA 2026/27 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 17, 2026

TUME YA UTUMISHI WA UMMA KUIMARISHA UKAGUZI NA MFUMO WA RUFANI KUPITIA TEHAMA 2026/27



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, imetangaza mpango wa kuimarisha usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma kwa kuongeza ukaguzi wa taasisi, kushughulikia rufaa kwa ufanisi zaidi na kuboresha mifumo ya kidijitali katika mwaka wa fedha 2026/27.

Hayo yameelezwa Aprili 17, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani J. Kikwete, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Waziri Kikwete amesema katika kipindi hicho Tume hiyo itafanya mikutano minne ya kisheria itakayoshughulikia rufaa, malalamiko na masuala mbalimbali ya kiutumishi, kwa lengo la kuhakikisha haki na uwazi vinazingatiwa katika utumishi wa umma.

Aidha, Tume ya Utumishi wa Umma imepanga kufanya ukaguzi wa kawaida katika taasisi 300 za umma pamoja na ukaguzi maalum katika taasisi 10, ili kuangalia uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa rasilimaliwatu.

Katika kuongeza uelewa wa watumishi, taasisi 574 zitapatiwa elimu kuhusu majukumu ya Tume na namna ya kuzingatia sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Serikali pia itaendeleza maboresho ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Rufaa, Malalamiko na Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria (PSCMIS), hatua inayolenga kuongeza ufanisi na uwazi katika utoaji wa haki kwa watumishi wa umma.

Vilevile, Tume hiyo itaendelea kufuatilia na kuhakiki vielelezo vya rufaa na malalamiko kutoka kwa warufani na mamlaka za nidhamu, ili kuhakikisha maamuzi yanayotolewa yanazingatia sheria na haki.

Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Tume ya Utumishi wa Umma itashirikiana na taasisi nyingine barani Afrika na katika ukanda wa SADC, sambamba na kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kushughulikia mashauri ya watumishi yanayofikishwa mahakamani.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Tume ya Utumishi wa Umma imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 12.85, ambapo asilimia 96.11 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na asilimia 3.89 kwa miradi ya maendeleo.

Serikali imesema hatua hizo zinalenga kuimarisha uwajibikaji, haki na ufanisi katika utumishi wa umma kupitia mifumo ya kisasa ya usimamizi na TEHAMA.

No comments:

Post a Comment