OFISI YA WAZIRI MKUU YAINOA TIMU YA KUKABILIANA NA MAAFA MKOA WA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 27, 2026

OFISI YA WAZIRI MKUU YAINOA TIMU YA KUKABILIANA NA MAAFA MKOA WA DODOMA





Na Mwandishi wetu- DODOMA

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, amesema Ofisi yake ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa ipo katika hatua ya kuanzisha Kituo cha Operasheni ya Dharura katika Mkoa ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004.

Dkt. Kazungu ameyasema hayo leo tarehe 27 Aprili,2026 jijini Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa Timu ya kukabiliana na dharura ya Mkoa ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa pamoja na uanzishaji wa kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura cha Mkoa.


Aidha, Dkt. Kazungu ameshukuru ujio wa elimu hiyo ndani ya Mkoa wa Dodoma akisema itasaidia kuwajenga kielimu Maafisa wa Mkoa ili waweze kupeleka elimu katika ngazi za Wilaya.


"Elimu hii itasaidia kuongeza ujuzi na weledi kwa Maafisa wa Mkoa kwani majanga haya yamekuwa na madhara mengi kwa jamii," alisema Dkt. Kazungu.


Pia, alisisitiza ukusanyaji wa taarifa kwa wakati na kabla ya majanga ili kurahihisisha kuyakabili pamoja na kuboresha mawasiliano ya karibu baina ya wananchi na Maafisa wa Mkoa.


"Lazima kuwepo ushirikiano baina yetu na Wananchi ili tuweze kupambana na maafa ndani ya Mkoa wetu wa Dodoma," alisisitiza.

Awali Kaimu Mkurugezi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Selestine Masalamadu aliupongeza Mkoa wa Dodoma kwa kuwa tayari kupokea elimu ya maafa na majanga na kusema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara hiyo ina jukumu la kuratibu shughuli za Kuzuia, Kupunguza Athari, Kujiandaa, Kukabiliana na Kurejesha hali baada ya maafa.

Vilvile, alisema kuwa Ofisi inaendelea kuratibu uanzishaji na uendeshaji wa Vituo vya Operesheni na Mawasiliano ya Dharura vya Mikoa pamoja na Timu za kukabiliana na dharura , ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamaizi wa Maafa ya Mwaka 2004, Sheria ya Usimamaizi wa maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake.


“Lengo la mafunzo haya ni kuimarisha uwezo wa Mkoa kuratibu shughuli za usimamaizi wa maafa ili kupunguza madhara wakati wa dharura. Mafunzo haya yatawajengea uwezo washiriki katika maandalizi, uratibu wa taarifa, mwitikio wa haraka, usimamizi rasilimali na utoaji wa huduma kwa waathirika,” alifafanua Kanali Masalamadu.


Aidha, alibainisha kwamba kila Mkoa unatakiwa kuwa na chumba maalum kwa ajili ya kuratibu shughuli za maafa na dharura huku akihimiza kuharakishwa kwa upatikanaji wa chumba chenye sifa stahiki kuwezesha uanzishwaji kamili wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Mkoa wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment