SEKTA YA TEHAMA YAONGEZA KASI YA UKUAJI UCHUMI, MCHANGO WA PATO LA TAIFA WAONGEZEKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

SEKTA YA TEHAMA YAONGEZA KASI YA UKUAJI UCHUMI, MCHANGO WA PATO LA TAIFA WAONGEZEKA


Na Okuly Julius ,OKULY BLOG,DODOMA


Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kuwa injini muhimu ya ukuaji wa uchumi nchini, baada ya takwimu kuonesha kuimarika kwa kasi ya ukuaji na mchango wake katika Pato la Taifa.


Hayo yamebainishwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027

 

Alisema kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2024, shughuli za habari na mawasiliano zilikua kwa asilimia 14.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.6 mwaka 2023.


Alieleza kuwa ongezeko hilo limetokana na upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano, kuongezeka kwa matumizi ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii, matumizi ya mikutano ya mtandaoni pamoja na ongezeko la huduma za malipo kupitia mitandao ya simu.


“Ukuaji huu umewezesha mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa kuongezeka kutoka asilimia 1.5 mwaka 2023 hadi asilimia 1.6 mwaka 2024, jambo linaloonesha namna TEHAMA inavyoendelea kuwa mhimili wa maendeleo ya uchumi wa kisasa,” alisema Waziri Kairuki.


Alibainisha kuwa sekta ya TEHAMA ni sekta wezeshi na mtambuka inayochochea utekelezaji wa shughuli za sekta nyingine kama elimu, afya, biashara na huduma za kifedha, hivyo kuifanya kuwa nguzo muhimu katika kufikia uchumi wa kidijitali.


Katika kuhakikisha mchango halisi wa sekta hiyo unapimwa kwa usahihi zaidi, Waziri Kairuki alisema Wizara inaendelea na maandalizi ya Akaunti ya Upimaji wa Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy Satellite Account – DESA), ambayo itapanua wigo wa upimaji wa mchango wa TEHAMA katika Pato la Taifa.


Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, wizara kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, imeanza kukusanya takwimu muhimu zitakazotumika katika uandaaji wa akaunti hiyo.


Kwa upande wa miundombinu, Waziri Kairuki alisema serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na minara ya mawasiliano, ambapo kata 688 zimefikishwa huduma kwa kujengwa kwa minara iliyowanufaisha wananchi takribani milioni 8.5.


Aidha, ufikishaji wa huduma za mkongo katika wilaya 86 umewezesha kurahisisha mawasiliano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi, huku ukisaidia pia utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi.


“Hatua hizi zimewezesha maeneo yaliyokuwa na changamoto za mawasiliano kufikiwa na huduma za uhakika, na hivyo kurahisisha shughuli za kiuchumi, kijamii na kiutawala kwa wananchi,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji katika TEHAMA ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za kidijitali, sambamba na kukuza uchumi wa taifa unaotegemea teknolojia na ubunifu.

No comments:

Post a Comment