Na WMMJWM Iringa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amewahimiza vijana nchini kuthubutu na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kuleta mapinduzi ya viwanda na maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza Aprili 30, 2026 wakati akifunga Kongamano lililowakutanisha wananchi na wataalamu mbalimbali katika chuo cha Maendeleo ya Jamiii Ruaha Mkoani Iringa, Dkt. Jingu amesema vijana wana nafasi kubwa ya kubadilisha jamii endapo watafungua macho na kubaini fursa zinazowazunguka na kuzitumia kwa ubunifu na vitendo.
“Vijana mna uwezo wa kuleta mapinduzi ya viwanda ikiwa watathubutu kuzigeuza changamoto kuwa fursa na kuleta suluhisho katika jamii zenu.” amesema Dkt. Jingu.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki na fursa mbalimbali zinazolenga kuwainua vijana na wanawake kiuchumi, hivyo ni wajibu wao kuzitumia kikamilifu huku akiwataka pia kuamini mawazo yao, kukuza fikra walizonazo na kuhakikisha ndoto zao zinageuka kuwa uhalisia kupitia ubunifu.
Katika Kongamano hilo, washiriki walipata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujadili ubunifu na mbinu za kujikwamua kiuchumi, huku wakihamasishwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Aidha, Dkt. Jingu ametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chuoni hapo, ikiwemo ile inayotumika kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kama vile ufugaji samaki, ushonaji wa nguo, viatu na kituo cha ubunifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ruaha Godfrey Mafungu amesema kongamano hilo limefanikiwa kuwakutanisha wadau muhimu wakiwemo Maafisa Maendeleo ya Jamii, Taasisi za fedha, wajasiriamali na wabunifu ili kushirikiana mawazo na mbinu za kukuza uchumi.
“Kongamano hili limeleta pamoja wadau mbalimbali ili kujadili ubunifu na kubainisha fursa zinazoweza kutumiwa kwa manufaa ya jamii.” amesema Mafungu.
Miongoni mwa vijana walionufuika na mkopo wa asilimia kumi Kassim Jeilan, ameeleza jinsi yeye na kikundi chake walivyofanikiwa kupata mkopo huo kupitia halmashauri ya Iringa na kuanzisha kiwanda kidogo cha kuchakata juisi za matunda.
“Tunashukuru Serikali na wataalamu waliotuongoza hadi tukapata mkopo wa shilingi milioni sita. Umetusaidia kuanzisha biashara, na sasa tunaendesha kiwanda kidogo cha juisi.” amesema Kassim.
Kongamano hilo ni chachu ya kuhamasisha vijana na wanawake kuchangamkia fursa zilizopo, kutumia ubunifu wao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.







No comments:
Post a Comment