WIZARA YA AFYA YAZINDUA KAMATI YA USHAURI WA RIJISTA YA SARATANI MBEYA KUTATUA CHANGAMOTO YA TAKWIMU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

WIZARA YA AFYA YAZINDUA KAMATI YA USHAURI WA RIJISTA YA SARATANI MBEYA KUTATUA CHANGAMOTO YA TAKWIMU


Wizara ya Afya leo imezindua kamati ya ushauri wa rejista ya saratani Mbeya hub kwa ajili ya usajili wa visa vya ugonjwa wa saratani, hatua inayolenga kupata takwimu sahihi zitakazosaidia maboresho ya huduma na utungaji wa sera za matibabu nchini (Population-Based Cancer Registry).

Akizindua kamati hiyo mkoani Mbeya, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCD) kutoka Wizara ya Afya, Edith Bakari, amesema kuwa mfumo huo wa ukusanyaji takwimu unakwenda kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa taarifa kamili kutoka vituo vya afya vya msingi.


“Licha ya mafanikio makubwa tunayoyaona kwenye hospitali za kanda na mikoa, bado kuna pengo la taarifa kutoka vituo vya msingi. Kamati hii inakwenda kuhakikisha takwimu zinakusanywa kwa ubora na kwa wakati ili kutusaidia katika kupanga sera sahihi za matibabu ya saratani.” – alisema Bi. Edith

Kwa upande wake, Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza mkoani Mbeya, Dkt. Reinfridy Chombo, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa, amesema uzinduzi huo ni mafanikio makubwa kwa mkoa wa Mbeya. Amewataka wataalamu waliochaguliwa kufanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha serikali kupanga mipango ya kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH), Dkt. Lazaro Mboma, ameishukuru serikali kwa hatua hiyo na kueleza kuwa uzinduzi wa Kamati hiyo ya Ushauri (Regional Advisory Committee for Cancer Registry) umekuja wakati muafaka ambapo hospitali hiyo inaendelea kutoa na kuboresha huduma za kibobezi za saratani.

 “Tunaishukuru wizara kwa jukumu hili muhimu. Tunatoa rai kwa wananchi kuendelea kujitokeza kupata huduma kwani serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa na wataalamu wa saratani hapa kanda ya nyanda za juu kusini.”

Uzinduzi huo ulioshirikisha wadau wa afya ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Vital Strategies, umehitimishwa kwa wito kwa wanakamati kufanya kazi kwa uadilifu ili Rejista ya Mbeya iwe kiungo madhubuti kati ya vituo vya huduma na mfumo wa taifa wa takwimu.

No comments:

Post a Comment