SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MAWASILIANO, WANANCHI MILIONI 15 WANUFAIKA NA MIRADI YA TEHAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MAWASILIANO, WANANCHI MILIONI 15 WANUFAIKA NA MIRADI YA TEHAMA


Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA


Serikali imeendelea kupata mafanikio makubwa katika sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambapo utekelezaji wa miradi mbalimbali umeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa mamilioni ya wananchi nchini.


Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027. 


Alisema katika kipindi cha uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sekta hiyo imepiga hatua kubwa, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa minara 758 katika kata 688.


Alisema pia serikali imefanikiwa kuongeza nguvu minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G na 4G katika kata 231, hatua ambayo imeongeza ubora wa mawasiliano na upatikanaji wa intaneti kwa wananchi.


“Miradi hii imekamilika kwa asilimia 100 na imefanikisha kuwafikia wananchi takribani milioni 8.5 kupitia minara mipya, huku minara iliyoboreshwa ikiwahudumia wananchi zaidi ya milioni 4.2,” alisema Waziri Kairuki.


Katika kuendeleza juhudi hizo, Waziri Kairuki alibainisha kuwa Wizara inaendelea kutekeleza Mradi wa Mawasiliano Vijijini unaohusisha ujenzi wa minara 636 katika kata 443. Kati ya minara hiyo, 456 sawa na asilimia 72 tayari imekamilika.


Alifafanua kuwa kati ya minara iliyokamilika, 342 tayari imewashwa na kutoa huduma kwa wananchi, huku minara 114 ikitarajiwa kuwashwa ifikapo Juni, 2026. Aidha, minara 180 iliyobakia inatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2026.


“Utekelezaji wa mradi huu utakapokamilika utawezesha wananchi takribani milioni 2.5 kufikiwa na huduma za mawasiliano, hasa katika maeneo ya vijijini ambayo awali hayakuwa na mtandao wa uhakika,” aliongeza.


Kwa upande wa miundombinu ya kitaifa, Waziri Kairuki alisema serikali imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika wilaya 86 nchini na kuunganisha nchi saba kati ya nane jirani, hatua inayoiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha mawasiliano ya kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Alisema juhudi zinaendelea kuiunganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mkongo huo, jambo litakaloongeza fursa za biashara, uwekezaji na mawasiliano ya kikanda.


Aidha, Wizara imeendelea kusimamia utekelezaji wa mradi wa Faiba Mlangoni unaolenga kusambaza huduma za intaneti ya kasi hadi kwa wananchi majumbani. Waziri Kairuki alisema hadi Machi 2026, jumla ya njia za maunganisho 132,793 zimekamilika kati ya 279,795 zilizopangwa.


Aliongeza kuwa hadi sasa, wateja 64,266 kati ya 126,740 waliolengwa wameunganishwa na huduma hiyo, sawa na asilimia 51 ya lengo lililokusudiwa.


Waziri Kairuki alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali jumuishi, kwa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za mawasiliano zenye ubora na gharama nafuu, hali itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

No comments:

Post a Comment