WIZARA YA MAWASILIANO YAVUKA LENGO LA MAKUSANYO KWA ASILIMIA 133.5 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

WIZARA YA MAWASILIANO YAVUKA LENGO LA MAKUSANYO KWA ASILIMIA 133.5




Na Okuly Julius ,OKULY BLOG,DODOMA


Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa maduhuli, baada ya kuvuka lengo lililowekwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa zaidi ya asilimia 30.

Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027

Alisema wizara ilikadiria kukusanya Shilingi 120,369,242,950 kupitia mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, lakini hadi kufikia Machi 2026 imefanikiwa kukusanya Shilingi 160,698,818,453.40, sawa na asilimia 133.5 ya lengo.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika miundombinu ya mawasiliano, hususan ujenzi na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao umefanikiwa kuunganisha wilaya 86 nchini na kuongeza uwezo wa usafirishaji wa data.

“Uboreshaji huu wa miundombinu umeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu na kwa uhakika zaidi, jambo lililochochea matumizi ya huduma za mkongo na hivyo kuongeza mapato ya serikali,” alisema Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alibainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, wizara imepokea na kutumia jumla ya Shilingi 147,768,795,246.62, sawa na asilimia 50.6 ya lengo lililokusudiwa kwa mwaka husika.

Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi 7,880,515,646.15 zilitumika kwa matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi 4,100,186,167 zilielekezwa kwenye mishahara ya watumishi, huku Shilingi 3,780,329,479.15 zikitumika kwa matumizi mengineyo ya uendeshaji.

Aidha, sehemu kubwa ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 139,888,279,600.47, zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo za maendeleo, Shilingi 55,406,701,365.02 ni fedha za ndani, huku Shilingi 84,481,578,235.45 zikiwa ni fedha kutoka vyanzo vya nje.

Waziri Kairuki alisisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea katika sekta ya mawasiliano utaendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa kidijitali, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, na kuongeza ushindani wa Taifa katika nyanja za teknolojia na ubunifu.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuhakikisha fedha zote zinazotengwa zinaleta tija inayokusudiwa kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment