
Na OWM - TAMISEMI, Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Jafar Seif amesema kuwa, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata za kimkakati kikiwemo kituo cha afya Nyamirembe ili kusogeza huduma za dharura na upasuaji kwa mama wajawazito.
Dkt. Seif amesema hayo leo Aprili 14, 2026 Bungeni Jijini Dodoma kwa Niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wakati akijibu swali la Mhe. Cornel Lucas Magembe Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini aliyetaka kujua ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa kituo cha afya Nyamirembe yalipo makao makuu ya tarafa.
Dkt. Seif ameanisha kuwa, katika mwaka wa fedha 2026/27 Serikali imetenga Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato kikiwemo kituo cha afya Iparamasa kilichotengewa Shilingi Milioni 108.
Dkt. Seif amesema, katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/26 Serikali imejenga na kuboresha jumla ya vituo vya afya vitano (5) katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa gharama ya Shilingi Bilioni 2.64.
Akieleza kuhusu fedha zilizotolewa kuboresha miundombinu, Dkt. Seif amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 Serikali imetoa jumla ya Shilingi Milioni 489 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika zahanati ya Kasenga na kuwa kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma za dharura za upasuaji.



No comments:
Post a Comment