SERIKALI KUZINDUA SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI 2025 DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 4, 2026

SERIKALI KUZINDUA SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI 2025 DODOMA


Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Alex Haraba, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Aprili 4, 2026 jijini Dodoma kuelekea uzinduzi Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, inayotarajiwa kuzinduliwa Aprili 8, 2026 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali kupitia Wizara ya Fedha inalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi zenye ubora unaotakiwa, kwa wakati na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha (Value for Money).

Katika kufikia azma hiyo, Serikali imeandaa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, inayotarajiwa kuzinduliwa Aprili 8, 2026 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 4, 2026 jijini Dodoma kuelekea uzinduzi huo, Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Alex Haraba, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, amesema uzinduzi wa sera hiyo ni hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kupitia mnyororo wa ugavi.

Amesema sera hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuweka mfumo jumuishi na wa kimkakati wa kusimamia shughuli zote za mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma.

Haraba amefafanua kuwa mfumo huo unahusisha hatua mbalimbali kuanzia upangaji wa mahitaji, ununuzi wa umma, uagizaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali, upokeaji na urejeshaji wa bidhaa au mali, uhifadhi na utunzaji, matumizi na usambazaji, hadi uondoshaji wa bidhaa, vifaa au mali za umma.

Aidha, amesema kupitia utekelezaji wa sera hiyo, Serikali inatarajia kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuongeza ufanisi katika miradi ya maendeleo, kupunguza upotevu wa rasilimali, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Uzinduzi wa sera hiyo unaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi, unaoongeza thamani ya rasilimali za ndani na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya Taifa.


No comments:

Post a Comment