
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu kupitia utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuongeza ubora wa elimu na kuendana na mahitaji ya karne ya 21.
Amesema hayo wakati akihitimisha Mkutano wa Pili wa Baraza la 37 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, ambapo alibainisha kuwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita zimeendelea kuleta mageuzi chanya katika sekta hiyo muhimu.
Ameeleza kuwa miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni uzinduzi wa Mkakati wa Kisayansi wa Kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) pamoja na Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri, hatua zinazolenga kuboresha ufundishaji na kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Pia amesisitiza umuhimu wa elimu ya amali katika kuwajengea vijana stadi na maarifa yatakayowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof.Carolyne Nombo, amesema kuwa utekelezaji wa kaulimbiu ya mkutano wa wafanyakazi ya “Ushirikishwaji na Mshikamano wa Wafanyakazi ni Chachu ya Kuimarisha Elimu Inayochochea Ubunifu” ni muhimu katika kufanikisha malengo ya sekta ya elimu nchini.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano kazini ni msingi wa kuleta mabadiliko ya kweli katika sekta ya elimu.
Ameeleza kuwa kaulimbiu hiyo inalenga kuwajenga watumishi kuwa na utamaduni wa kufanya kazi kwa pamoja, kwa bidii na kwa uwajibikaji, hali ambayo itachochea mageuzi makubwa yanayohitajika katika kuboresha ubora wa elimu nchini.
“Tunaposhirikiana na kufanya kazi kwa bidii kama timu moja, tunaweka msingi imara wa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, yanayoakisi dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050,” amesema Prof. Nombo.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuendana na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023), pamoja na kuzingatia mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika mitaala iliyoboreshwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya serikali katika kutekeleza majukumu yao, akibainisha kuwa nidhamu na uwajibikaji ni nguzo muhimu za kufanikisha malengo ya wizara.
Mkutano huo ulijadili mada mbalimbali ikiwemo bajeti ya Wizara, usimamizi wa rasilimaliwatu, maadili ya utumishi wa umma pamoja na afya ya akili mahali pa kazi, huku akisisitiza kuwa maarifa yaliyopatikana yatumike kuboresha utendaji kazi wa kila siku.








No comments:
Post a Comment