‎KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA AWAMU YA PILI KUANZA MEI 01-15, 2026 DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

‎KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA AWAMU YA PILI KUANZA MEI 01-15, 2026 DODOMA


‎Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amefanya Mkutano na waandishi wa habari kuutangazia Umma kuhusu kuanza kwa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kupitia Kampeni ya ‘Msaada wa Kisheria ya Mama Samia’ awamu ya Pili.

‎“Utekelezaji wa Kampeni hii ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha upatikanaji wa haki kupitia huduma za msaada wa kisheria kwa makundi yenye uhitaji zaidi hususan wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana”. Mhe. Senyamule.

‎Aliongeza kuwa, katika utekelezaji uliofanyika 2023, Mkoa ulipata bahati ya kuwa wa kwanza kuanza utekelezaji wa Kampeni hiyo yenye manufaa makubwa kwa wananchi kwani jumla ya wananchi 86,947 wakijumuisha Wanaume 42,298 na Wanawake 44,649 walifikiwa na kupatiwa huduma za Msaada wa Kisheria.

‎Aidha, kati ya migogoro 818 iliyopokelewa, migogoro 452 ilitatuliwa na migogoro 366 inaendelea kufanyiwa kazi. Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeona bado kuna uhitaji na umuhimu wa kuendeleza juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi na kwa wakati.

‎Kampeni hiyo itaanza rasmi Mkoa wa Dodoma Mei Mosi hadi 15, 2026 ambapo huduma zifuatazo zitatolewa bila malipo; ushauri wa kisheria, elimu ya masuala ya kisheria, uandaaji wa nyaraka za kisheria, uwakilishi Mahakamani na katika Mabaraza kwa wananchi wenye mashauri au wanaotaka kufungua mashauri, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na huduma ya usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kupitia RITA.

Elimu kwa jamii itatolewa katika ngazi ya Wilaya,Kata, Mitaa/Vijiji sambamba na kufanyika katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya wananchi kama vile masoko, vituo vya mabasi, mikusanyiko ya kijamii na taasisi za elimu. Aidha, kutakuwa na vituo vya huduma katika maeneo yafuatayo:-

‎Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kituo kitakuwa Uwanja wa Mtekelezo, mkabala na Msikiti wa Gadaf;

‎Halmashauri ya Wilaya Chamwino vituo vitakuwa katika Ofisi ya Kijiji Buigiri, Kata ya Chinangali na Ofisi ya Kata Mlowa Barabarani;

‎Halmashauri ya Wilaya Kongwa vituo vitakuwa katika Ofisi ya Kata ya Kibaigwa na Ofisi ya Kata ya Mkoka;

‎Halmashauri ya Wilaya Mpwapwa vituo vitakuwa katika Ofisi ya Kata ya Mpwapwa Mjini na ofisi ya Kata ya Kibakwe;

‎Halmashauri ya Wilaya Bahi vituo vitakuwa eneo la Mwachubu senta, Kata ya Bahi Mjini;

‎Halmashauri ya Wilaya Chemba kituo kitakuwa Kata ya Chemba katika Ofisi ya Kijiji Chemba;

‎Halmashauri ya Mji Kondoa kituo kitakuwa eneo la Stendi ya Zamani; na

‎Na Halmashauri ya Wilaya Kondoa kituo kitakuwa Eneo la Pahi Senta katika Kata ya Pahi.

‎Mkuu wa Mkoa amewasihi Waanchi kujitokeza kwa wingi, wakati wote wa utekelezaji wa Kampeni ili waweze kupata huduma za msaada wa kisheria bure na huduma nyingine zinazotolewa kupitia Kampeni hiyo kwani kupata haki ni haki ya msingi ya binadamu na kila mtu anastahili ulinzi wa haki yake.

‎Kauli Mbiu ya Kampeni hiyo ni, “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo” ambayo ina akisi maono ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka, 2050 inayolenga kujenga jamii yenye usawa, haki na ustawi wa wote.

No comments:

Post a Comment