
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Minara ya mawasiliano 9,124 imejengwa nchini kufikia Machi 2026, ambapo kati yake minara 1,653 imejengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), hatua iliyowezesha huduma za simu na intaneti kuwafikia takribani wananchi milioni 46.
Aidha, watoa huduma za mawasiliano wakiwemo Airtel, Vodacom, Halotel, TTCL na Honora wamechangia takribani asilimia 60 ya gharama za ujenzi wa kila mnara wa mawasiliano, hali inayoendelea kuimarisha kasi ya upanuzi wa miundombinu ya TEHAMA nchini.
Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema mchango wa sekta binafsi umewezesha kuimarika kwa huduma za intaneti kupitia maunganisho ya Mkongo wa Taifa hadi kwa mtumiaji wa mwisho (Last Mile Connectivity), hatua inayoongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali majumbani, mashuleni na maeneo ya umma.
Ameongeza kuwa sekta hiyo pia imechangia katika kukuza uchumi kupitia utoaji wa mikopo kwa biashara ndogo na za kati, ajira, pamoja na kufungua fursa za biashara mtandao, hatua inayosaidia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali 2024–2034.

No comments:
Post a Comment