
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, akizungumza na akieleza Utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na Mwelekeo 2026/27 wa taasisi hiyo katika mkutano na waandishi wa habari , Agosti 19,2026 jijini Dodoma.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , Dodoma
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amesema zaidi ya wananchi 200,000 katika mikoa 15 nchini wamefikiwa na huduma za uchunguzi wa awali wa saratani kupitia kampeni ya Tiba Mkoba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma za uchunguzi karibu na wananchi na kuongeza uwezekano wa kugundua ugonjwa huo mapema.
Dkt. Msemo amesema hayo Agosti 17,2026 jijini Dodoma, wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na Mwelekeo wa Mwaka wa Fedha 2026/27 wa ORCI, akieleza kuwa kampeni hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu saratani na kuwafikia wananchi ambao wanaweza kuwa na changamoto ya kufika katika vituo maalumu vya huduma.
Amesema kupitia kampeni hiyo, ORCI imefika katika mikoa 15 na maeneo mbalimbali ya kazi, ambako zaidi ya watu 200,000 wamepatiwa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani.
Kwa mujibu wa Dkt. Msemo, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa ORCI wa kuimarisha kinga, elimu kwa umma na uchunguzi wa mapema, hususan kwa saratani za matiti, mlango wa kizazi na tezi dume, hatua ambayo inalenga kuongeza uwezekano wa wagonjwa kupata matibabu kwa wakati.
Akizungumzia dhana potofu iliyopo katika jamii kwamba saratani haina tiba, Dkt. Msemo amesisitiza umuhimu wa wananchi kuachana na dhana hiyo na badala yake kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.
“Ninawaomba wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kwani ugonjwa wa saratani unatibika kama magonjwa mengine,” amesema Dkt. Msemo.
Amesema kuimarishwa kwa huduma za uchunguzi wa mapema ni muhimu katika kupunguza vifo vinavyotokana na kuchelewa kugundua saratani.
Dkt. Msemo amesema mafanikio ya kuwafikia wananchi yanaenda sambamba na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu, vifaa tiba na teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu ya saratani.
Ametaja Kituo cha Saratani Mbeya kuwa miongoni mwa miradi hiyo, ambapo ujenzi umefikia takribani asilimia 57, huku mradi ukiwa na thamani ya Sh bilioni 11.
Amesema ujenzi unatarajiwa kukamilika Januari 2027, huku kituo hicho kikitarajiwa kuanza kutoa huduma Julai 2027. Kitakapokamilika, kituo hicho kitahudumia wananchi wa Mbeya na maeneo ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na wagonjwa kutoka Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akizungumzia teknolojia mpya, Dkt. Msemo amesema Serikali imewekeza Sh bilioni 18.2 katika mashine ya PET Scan, inayotumika kusaidia kugundua saratani na kuonesha iwapo ugonjwa umesambaa katika maeneo mengine ya mwili.
Amesema PET Scan pia hutumika katika uchunguzi wa baadhi ya magonjwa ya ubongo na moyo, huku Tanzania ikiwa nchi ya kwanza katika Afrika Mashariki na Kati kuwa na mashine hiyo.
Aidha, amesema ORCI imefungwa mashine ya kisasa ya tiba ya mionzi aina ya ELEKTA Harmony, iliyogharimu Sh bilioni 8.3.
Kwa mujibu wa Dkt. Msemo, mashine hiyo inatumia teknolojia ya Image Guided Radiotherapy (IGRT) inayowezesha wataalamu kutoa tiba ya mionzi kwa usahihi mkubwa kwa kuzingatia eneo halisi la uvimbe, huku ikilinda kwa kiwango kikubwa tishu na viungo vyenye afya vilivyo karibu na eneo linalotibiwa.
Dkt. Msemo amesema ORCI pia imenunua mashine mbili za Mammography zenye thamani ya takribani Sh bilioni 1.1, ambazo zitaongeza uwezo wa Taasisi kufanya uchunguzi wa kina wa saratani ya matiti.
Amesema uwepo wa mashine hizo utasaidia kuongeza uwezo wa kugundua mabadiliko ya saratani katika hatua za awali, hivyo kuwawezesha wagonjwa kupata uchunguzi sahihi na kuanza matibabu kwa haraka zaidi.
Katika tiba ya mionzi, Dkt. Msemo amesema ORCI imekamilisha kwa asilimia 100 mradi wa Linear Accelerator uliogharimu takribani Sh bilioni 7.9.
Amesema kati ya fedha hizo, takribani Sh bilioni 7.3 zilitumika katika ununuzi na usimikaji wa mashine hiyo, huku Sh milioni 800 zikitumika katika ujenzi na ukarabati wa chumba maalumu cha mashine.
Amesema huduma za matibabu kwa kutumia mashine hiyo tayari zimeanza kutolewa, huku lengo likiwa kuongeza uwezo wa ORCI kuhudumia wagonjwa wengi zaidi na kupunguza muda wa kusubiri matibabu ya mionzi hadi wastani unaolengwa wa takribani wiki mbili.
Dkt. Msemo amesema ORCI inaendelea na maandalizi ya kuanzisha vituo vipya vya saratani katika Mtwara, Kigoma na Arusha, hatua inayolenga kusogeza huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi.
Amesema miradi hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa wagonjwa kusafiri hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kupata baadhi ya huduma za saratani.
Aidha, amesema ORCI ina mpango wa kuwezesha kuanzishwa kwa uzalishaji wa dawa na bidhaa mbalimbali zinazotumika katika matibabu ya saratani nchini, kwa lengo la kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa bidhaa muhimu za matibabu.

No comments:
Post a Comment