SERIKALI imeonya kuwa mtu au taasisi itakayobainika kuharibu au kutenda kosa dhidi ya Miundombinu Muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CII) atakabiliwa na adhabu kali kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amesema hayo leo Jumatano Agosti 19, 2026 jijini Dar es Salaam ambapo ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria hiyo, mhusika anaweza kutozwa faini isiyopungua Shilingi milioni 100, au mara tatu ya hasara iliyosababishwa, au kifungo kisichopungua miaka mitano.
Amesema adhabu hizo zinaweza pia kutolewa kwa pamoja, ikiwemo faini na kifungo, kulingana na kosa lililofanyika dhidi ya CII.
Waziri Kairuki amesema hatua hizo ni sehemu ya mfumo wa kisheria wa kulinda miundombinu ambayo kutofanya kazi kwake kunaweza kusababisha madhara au athari za kiusalama, kiuchumi na kijamii.
Amesema changamoto au vitisho vyovyote vya kiusalama vinavyohusu CII lazima vitolewe taarifa kwa mamlaka za udhibiti ndani ya saa 24 tangu kubainika kwake.
Taarifa hiyo inatakiwa kueleza muda ambao tukio limetokea, aina ya athari iliyojitokeza, huduma zilizoathirika pamoja na hatua za awali zilizochukuliwa.
Kwa mujibu wa Waziri, Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya umma na binafsi imebainisha CII na kuandaa miongozo mitano kwa ajili ya kuimarisha usimamizi na ulinzi wake.
Miongozo hiyo inahusu utambuzi na usimamizi wa CII, ukaguzi, tathmini ya hatari, uhakika na uhalisia wa data pamoja na mipango ya urejesho wa huduma baada ya janga.
CII inahusisha sekta za habari na mawasiliano, fedha na benki, maji, afya, nishati, madini, usafirishaji, chakula na kilimo, ujenzi, uchumi wa buluu, mazingira, viwanda, ulinzi, anga, elimu, utawala wa kiserikali, ulinzi wa raia, ardhi na usalama au utulivu wa umma.
Waziri Kairuki amesema hatua za usajili wa CII zinaendelea kupitia CII Portal, baada ya Tangazo la Serikali Na. 147 la Juni 19, 2026 kutangaza rasmi miundombinu hiyo kwa ajili ya usajili na kupata ulinzi wa kisheria.

No comments:
Post a Comment