TANROADS YAWATAKA WANANCHI KUWA MAKINI DHIDI YA MATAPELI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 2, 2026

TANROADS YAWATAKA WANANCHI KUWA MAKINI DHIDI YA MATAPELI


Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetoa tahadhari kwa umma kuhusu kuwepo kwa matapeli wanaojifanya watumishi wa wakala huo, hususan katika Mkoa wa Dodoma, na kuwalaghai wananchi kwa njia ya simu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, matapeli hao wamekuwa wakiwasiliana na wamiliki wa mabango ya matangazo (billboards), wakijitambulisha kama maafisa wa TANROADS na kudai malipo ili kuzuia mabango yao kuondolewa kwa madai ya kuvuka muda wa vibali.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya wananchi tayari wameathirika baada ya kutuma fedha kwa watu hao, wakiamini kuwa wanawasiliana na watumishi halali wa TANROADS.

“TANROADS haitoi huduma wala kupokea malipo kupitia namba binafsi za simu au kwa mtu mmoja mmoja. Malipo yote hufanyika kupitia mifumo rasmi ya Serikali inayotambulika,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wametakiwa kuwa makini na kuepuka kutuma fedha kwa mtu yeyote anayewasiliana nao kwa njia zisizo rasmi akijitambulisha kama mtumishi wa wakala huo.

Aidha, TANROADS imesema inaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wa vitendo hivyo vya utapeli.

Wananchi pia wamehimizwa kutoa taarifa za matukio ya aina hiyo katika ofisi za TANROADS zilizo karibu au kupitia njia rasmi za mawasiliano za wakala huo.


Wakala huo umeeleza kuwa utaendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha huduma zake zinatolewa kwa uwazi, usalama na uadilifu.

No comments:

Post a Comment