TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA USAFIRISHAJI KIKANDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 14, 2026

TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA USAFIRISHAJI KIKANDA


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa majadiliano yaliyoandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu nafasi ya shoroba za usafirishaji (transport corridors) katika kukuza uchumi wa Afrika, pembezoni mwa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na IMF (2026 IMF/WBG Spring Meetings) inayoendelea jijini Washington D.C, ambapo alisema Tanzania itaendelea kujipambanua kama kitovu muhimu cha usafirishaji na uchumi wa kikanda barani Afrika, kufuatia juhudi zake za kuendeleza na kuboresha shoroba za usafirishaji zinazochochea biashara, ajira na ushirikiano wa nchi jirani.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), akizungumza wakati wa majadiliano yaliyoandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu nafasi ya shoroba za usafirishaji (korido) katika kukuza uchumi wa Afrika, pembezoni mwa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na IMF (2026 IMF/WBG Spring Meetings) inayoendelea jijini Washington D.C, ambapo alisema Tanzania itaendelea kujipambanua kama kitovu muhimu cha usafirishaji na uchumi wa kikanda barani Afrika, kufuatia juhudi zake za kuendeleza na kuboresha shoroba za usafirishaji zinazochochea biashara, ajira na ushirikiano wa nchi jirani. Wengine katika picha ni pia Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop (Katikati), na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Zarau Wendeline Kibwe (kushoto).


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-Washington D.C)


Na. Joseph Mahumi, WF, Washington D.C


Tanzania imeendelea kujipambanua kama kitovu muhimu cha usafirishaji na uchumi wa kikanda barani Afrika, kufuatia juhudi zake za kuendeleza na kuboresha shoroba za usafirishaji (transport corridors) zinazochochea biashara, ajira na ushirikiano wa nchi jirani.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati aliposhiriki mjadala ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu nafasi ya shoroba za usafirishaji katika kukuza uchumi wa Afrika, pembezoni mwa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na IMF (2026 IMF/WBG Spring Meetings) inayoendelea jijini Washington D.C.

Akizungumza katika jopo hilo, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuunganisha nchi za ukanda kupitia miundombinu ya kisasa, ikiwemo reli ya TAZARA iliyoanzishwa tangu miaka ya 1970 ambayo ni moja ya shoroba za awali za usafirishaji kati ya Tanzania na Zambia.

Mhe. Balozi Omar alibainisha kuwa, kwa muda mrefu shoroba hiyo ilitumika zaidi kwa usafirishaji pekee bila kunufaisha ipasavyo maendeleo ya kiuchumi katika maeneo inayopita, jambo ambalo sasa linafanyiwa kazi kupitia mpango wa kuibadilisha kuwa shoroba ya uchumi.

“Mwelekeo mpya ni kuhakikisha shoroba hizi zinakuwa za kiuchumi badala ya kuwa za usafirishaji pekee, hatua itakayochochea maendeleo ya viwanda, biashara na huduma kwa kuwa shoroba hizi ni muhimu si tu kwa maendeleo ya miji, bali pia kwa kuinua uchumi wa vijijini ambako uzalishaji mkubwa unafanyika na pia kuunganisha maeneo hayo na masoko kutafungua fursa kubwa za maendeleo,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha Mhe. Balozi Omar, alitaja pia mafanikio ya shoroba ya kati inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani kupitia Maziwa ya Victoria na Tanganyika, kuwa miundombinu hiyo imefungua milango ya biashara kwa nchi za Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Sudan Kusini, hatua ambayo imeimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Aliongeza kuwa katika kuimarisha zaidi nafasi hiyo, Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika Reli ya Kisasa (SGR), yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 10.2, ambayo imegawanywa katika vipande sita ndani ya nchi na mipango inaendelea kupanua reli hiyo hadi kufikia nchi za Burundi na DRC, hatua itakayoongeza zaidi mtandao wa usafirishaji na biashara katika ukanda wake.

“Uwekezaji huu unaenda sambamba na mkakati wa kukuza viwanda kupitia usindikaji wa mazao ya kilimo na madini, ili kuongeza thamani ya uzalishaji wa ndani na kuimarisha uchumi wa Taifa, ambapo sekta ya utalii itanufaika pia kwa kiasi kikubwa kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu hiyo, hatukusubiri mipango ya kikanda kuanza, tulianza sisi kama nchi tukitambua wajibu wetu wa kuchochea maendeleo ya ukanda” aliongeza Mhe. Balozi Omar.

Alisema kuwa hatua hizo zinaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati kama kitovu cha usafirishaji wa kikanda, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu barani Afrika.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, alisisitiza umuhimu wa kubadilisha mtazamo kutoka dhana ya muda mrefu ya kuwa na shoroba za usafirishaji (transport corridors) kwenda kwenye shoroba za kiuchumi kama ambavyo shoroba ya Dar es Salaam (Central Corridor), ilivyo na mchango mkubwa katika kuunganisha nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kusini.

Aliongeza kuwa shoroba za kiuchumi zina nafasi kubwa ya kuwa kichocheo cha uundaji wa ajira, kuongeza ushindani wa kiuchumi, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

“Licha ya umuhimu wa shoroba hizi, kuna haja ya kuangalia upya mfuatano wa uwekezaji wake, Kwa kawaida, nchi za pwani ndizo huanza kuwekeza kwanza kabla ya nchi zisizo na bandari kufuata, lakini wanufaika wakubwa wa awali ni nchi hizo zisizo na bandari, Hivyo, napendekeza umuhimu wa kubadili mtazamo huo au angalau kuweka mkazo kwenye upangaji sahihi wa uwekezaji, ili kuhakikisha manufaa yanaanza kuonekana mapema kwa wote.” Alisema Bw. Diop

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutumia kikamilifu maarifa na ushirikiano katika kuendeleza shoroba za uchumi zenye kasi, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuchochea biashara na ukuaji wa uchumi wa kikanda.

Alisema kuwa pamoja na kuanzisha shoroba hizo, ni lazima kuwepo kwa mazingira rafiki ya biashara yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu na kunufaika na fursa zinazotokana na uwekezaji huo.

Aidha, Dkt. Kibwe alisema kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika kujumuisha maendeleo ya shoroba za uchumi katika mipango na mikakati yao ya kitaifa ili kuhakikisha zinachangia moja kwa moja katika maendeleo ya kiuchumi.

Aliongeza kuwa uwekezaji katika shoroba hizo unaweza kusaidia kupunguza changamoto za udhaifu wa kiuchumi na kijamii, huku akisisitiza haja ya kuhakikisha mifumo ya shoroba inakuwa shirikishi na inayoweza kuunganishwa kikanda.

Dkt. Kibwe alisisitiza pia umuhimu wa taasisi za kifedha za kimataifa, ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika, katika kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali za kugharamia miradi hiyo mikubwa, ambayo ni msingi wa juhudi za Afrika kuelekea katika mapinduzi ya viwanda na kujitegemea kiuchumi.

No comments:

Post a Comment