WANAOHODHI LESENI ZA MADINI WATIKISWA, 40 ZAFUTWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 15, 2026

WANAOHODHI LESENI ZA MADINI WATIKISWA, 40 ZAFUTWA



Na Boniphace JOHN, OKULY BLOG - Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya madini imeiagiza tume ya madini kufuta leseni 40 na kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara za leseni na kuchukua hatua stahiki za kufuta leseni zote ambazo zitabainika kutokuendelezwa.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma April 15, mwaka huu waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema licha ya ongezeko la utoaji wa
leseni za madini nchini, kuna baadhi ya wamiliki wa leseni ambao wamekuwa
hawatekelezi wajibu wao wa umiliki wa leseni ikiwa ni pamoja na
kutokuziendeleza leseni wanazomiliki ndani ya muda uliotolewa kwa mujibu wa
Sheria.

Amesema wamiliki hao wamekuwa wanahodhi maeneo hawalipi ada stahiki za
leseni ambapo vitendo hivyo vimekua vikichangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa vitendo vya uchimbaji madini usio rasmi
vinavyotokana na uvamizi wa leseni hizo.

" Vitendo hivyo havivumiliki na Serikali
itaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na kufuta leseni zote ambazo
zitabainika kuwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuendelezwa ndani ya muda uliotolewa katika Sheria ya Madini Sura 123.

Aidha amesema April 10 , 2026 Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imetoa
hati za makosa kwa leseni nyingine 43 zikikujumuisha leseni 40 za utafutaji
madini na leseni tatu (3) za uchimbaji wa kati wa madini.

"Naielekeza Tume ya Madini kuendelea na zoezi la utoaji wa hati za makosa na endapo wamiliki wake watashindwa kurekebisha makosa ndani ya siku 30, leseni hizo zifutwe ili maeneo hayo yatolewe kwa wawekezaji wengine,"amesema Mavunde

Hata hivyo amesema kuwa Serikali imeendelea kufuatilia
kwa karibu mwenendo wa matukio ya milipuko ya madini ya dhahabu (gold
rush) katika maeneo mbalimbali nchini, na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la
kulinda usalama, kudumisha utulivu, na kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na
kanuni za madini.

"Kutokana na hali hiyo, natoa onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi chochote kinachojihusisha na uvamizi wa maeneo yenye leseni halali kwa
kigezo cha kuifanya kuwa gold rush tabia hiyo inakemewa vikali na
kuanzia sasa ni marufuku kuvamia maeneo ya leseni za madini kwa
sababu yoyote ile. Utaratibu wa utoaji wa leseni za madini upo wazi katika
Sheria yetu ya Madini na Kanuni zake na ni lazima ufuatwe,"amesema Mavunde

Vitendo vya watu kukimbilia maeneo yenye Taarifa za uwepo wa madini na kuanza uchimbaji bila leseni ni kinyume cha Sheria za jamuhuri ya muungano wa Tanzania ,Shughuli zozote za uchimbaji wa madini zinapaswa kufanyika Kwa kuzingatia umiliki wa leseni.

No comments:

Post a Comment