Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Wizara ya Katiba na Sheria imeomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 774.79 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha upatikanaji wa haki nchini.
Akiwasilisha hotuba hiyo bungeni jijini Dodoma Aprili 24, 2026, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amesema fedha hizo zitahudumia Wizara, Mhimili wa Mahakama pamoja na taasisi zake ili kuhakikisha utoaji wa haki unakuwa wa haraka na wenye ufanisi zaidi.
Katika mgawanyo wa bajeti hiyo, Dkt. Homera ameeleza kuwa shilingi bilioni 636.56 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku shilingi bilioni 137.42 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha miundombinu na huduma za kisheria.
Amesisitiza kuwa moja ya vipaumbele vikuu ni kusogeza huduma za msaada wa kisheria hadi ngazi ya jamii, hatua inayolenga kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa wa maeneo ya vijijini na pembezoni ambao mara nyingi hukosa huduma hizo muhimu.
Aidha, wizara imepanga kuandaa Sera ya Taifa ya Haki Madai pamoja na Mpango Kabambe wa Sekta ya Sheria, ikiwa ni jitihada za kuweka mfumo thabiti na wa kisasa utakaoratibu utoaji wa haki kwa ufanisi nchini.
Katika kuimarisha uelewa wa sheria, serikali pia itatoa elimu kwa wadau na umma kuhusu sera za haki jinai na msaada wa kisheria, sambamba na kuendesha kampeni za elimu ya Katiba na uraia ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao.
Vilevile, wizara inalenga kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR), hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, serikali imeweka mkazo kwenye usimamizi wa mirathi, usajili wa wosia na uanzishaji wa rejista ya watoa huduma za ufilisi, pamoja na kutoa mafunzo ya ubobezi kwa wataalamu wa sheria ili kuchochea mageuzi na ufanisi katika sekta hiyo.






No comments:
Post a Comment