
Wizara ya Madini imeendelea kuongeza uwekezaji katika tafiti za kina za madini kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za rasilimali za nchi na kuongeza tija katika sekta ya madini.
Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026 /2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, alisema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imefanya tafiti za jiofizikia kwa kutumia ndege nyuki katika maeneo ya Geita, Manyara na Lindi.
Alieleza kuwa tafiti hizo zimewezesha kubaini taarifa muhimu za kijiolojia pamoja na kuonyesha uwezekano wa kutumia teknolojia ya ndege nyuki katika utafiti wa madini, hususan kwa wachimbaji wadogo nchini.
Aidha, Wizara imekamilisha maandalizi ya kumpata mkandarasi wa kufanya utafiti wa kina katika vitalu viwili vya kimkakati kusini-magharibi mwa Tanzania, vinavyokadiriwa kufikia asilimia 18 ya eneo lote la nchi.
Mhe. Mavunde alisema hatua hiyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa taarifa za jiofizikia kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 34, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi wa utafutaji wa madini.
Katika kuhakikisha taarifa za madini zinapatikana kwa urahisi, Wizara kupitia GST inaendelea na ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi na Usambazaji wa Taarifa za Jiosayansi, ambao umefikia asilimia 45 ya utekelezaji wake.
Kwa upande wa wachimbaji wadogo, Wizara imetoa leseni 8,878 za uchimbaji mdogo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na rasilimali madini.
Aidha, STAMICO imeendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa wachimbaji wadogo kupitia huduma za uchorongaji, utafiti na uchenjuaji, ambapo mita 3,896.59 zimechimbwa kwa ajili ya utafutaji wa dhahabu.
Wizara pia imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kusafisha chumvi katika eneo la Nangurukuru, Kilwa, hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya madini ya chumvi nchini.
Kwa upande wa maendeleo ya wachimbaji wadogo, Serikali imeendelea kutenga maeneo maalum 99 kwa ajili ya uchambuzi na uwezeshaji, huku maeneo mengine mawili yakiwa tayari yameanza kutoa leseni kwa wachimbaji.
Vilevile, Wizara imeendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kushiriki mafunzo na ziara za kimataifa, ambapo wachimbaji 31 walitembelea Uturuki kujifunza teknolojia za kisasa za uchimbaji.
Katika kuimarisha upatikanaji wa mitaji, Wizara kupitia Tume ya Madini imesaini makubaliano na Benki ya CRDB yatakayowezesha upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo, ikiwa ni pamoja na kikundi cha Songwe Gold Family kinachotarajiwa kupata mkopo wa shilingi bilioni 50.
Kwa ujumla, Wizara ya Madini imesema inaendelea kuimarisha tafiti za kina, kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuboresha taasisi zake ili kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.

No comments:
Post a Comment