SERIKALI YAIMARISHA UWEKEZAJI NA UONGEZAJI THAMANI SEKTA YA MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 27, 2026

SERIKALI YAIMARISHA UWEKEZAJI NA UONGEZAJI THAMANI SEKTA YA MADINI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhamasisha uwekezaji na kuongeza thamani ya madini nchini kupitia mikakati mbalimbali inayolenga kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania.

Akiwasilisha taarifa hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, alisema Wizara imekuwa ikitangaza fursa za uwekezaji na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, ziara za viongozi pamoja na mikutano ya kitaifa na kimataifa.

Alieleza kuwa katika juhudi hizo, Wizara ilishiriki katika makongamano na maonesho nane ya kimataifa ikiwemo Future Minerals Forum ya Saudi Arabia, Mining Indaba ya Afrika Kusini na ZIMEC ya Zambia, hatua iliyosaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.

Aidha, ndani ya nchi Wizara iliandaa na kushiriki maonesho matano ikiwemo ya Sabasaba Dar es Salaam, Maonesho ya Biashara Zanzibar na maonesho ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini yaliyofanyika Geita.

Mhe. Mavunde alisema juhudi hizo zimeongeza mwamko wa uwekezaji na kuimarisha taswira ya Tanzania kama kitovu cha uwekezaji wa madini katika ukanda wa Afrika.

Aliongeza kuwa Serikali imekamilisha Mkakati wa Uongezaji Thamani Madini unaolenga kuondokana na uuzaji wa madini ghafi na badala yake kuhamasisha uuzaji wa madini yaliyoongezewa thamani ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, utekelezaji wa mkakati huo utachochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira, kuboresha ujuzi na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa.

Aidha, Wizara inaendelea kusimamia viwanda sita vya kusafisha dhahabu vilivyopo katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Geita na Mwanza, pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuyeyusha madini ya metali.

Vilevile, juhudi zinaendelea kuimarisha uongezaji thamani wa madini ya vito kupitia ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Jemolojia Tanzania, hatua inayolenga kuongeza utaalamu na ushindani wa bidhaa za madini katika soko la kimataifa.

No comments:

Post a Comment