TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUONGEZA MATUMIZI YA KIDIJITALI KURAHISISHA HUDUMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 17, 2026

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUONGEZA MATUMIZI YA KIDIJITALI KURAHISISHA HUDUMA


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete, amezitaka Taasisi za Umma kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kurahisisha utendaji kazi, kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akifungua rasmi Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali leo Juni 17, 2026, jijini Dodoma, Waziri Kikwete amesema maadhimisho hayo yanalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kuhimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali na kupokea mrejesho kutoka kwa wadau ili kuboresha huduma za umma.

Amesema watumishi wa umma wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na amewahimiza kutumia maadhimisho hayo kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za utoaji huduma na kuendelea kujenga utumishi wenye tija na uwajibikaji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Juma Mkomi amesema taasisi 225 zinashiriki maadhimisho ya mwaka huu, ikilinganishwa na taasisi 146 zilizoshiriki mwaka 2025, hali inayoonesha kuongezeka kwa mwitikio wa taasisi za umma katika kuwaletea wananchi huduma na taarifa muhimu.

Akizungumzia Kaulimbiu amesema imelenga katika maudhui ya ushiriki wa Serikali, taasisi binafsi na kamii.

Miongoni mwa washiriki wa maonesho hayo ni Wizara ya Madini na taasisi zake, ambazo zinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa, fursa za uwekezaji katika sekta ya madini na mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi.

Aidha, Kituo Cha Jemolojia Tanzania (TGC) kimeendelea kutoa elimu kuhusu uongezaji thamani wa madini ya vito na miamba pamoja na mafunzo mbalimbali yanayolenga kuongeza ujuzi na ushiriki wa watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini.

Maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: "Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu" 

No comments:

Post a Comment