WIZARA YA MADINI YAVUKA MALENGO YA MAKUSANYO, UTEKELEZAJI WA BAJETI WAIMARIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 27, 2026

WIZARA YA MADINI YAVUKA MALENGO YA MAKUSANYO, UTEKELEZAJI WA BAJETI WAIMARIKA


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA 


Wizara ya Madini imesema imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwemo kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli na kuimarisha shughuli za usimamizi wa rasilimali madini nchini.

Akiwasilisha taarifa hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, alisema Bunge lilikuwa limeidhinisha jumla ya shilingi bilioni 224.98 kwa ajili ya wizara hiyo, ambapo shilingi bilioni 100.38 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 124.60 kwa miradi ya maendeleo.

Alieleza kuwa hadi kufikia Machi 2026, Wizara ilikuwa imepokea shilingi bilioni 82.90, zikiwemo shilingi bilioni 72.43 kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 10.48 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Katika eneo la ukusanyaji wa maduhuli, Mhe. Mavunde alisema Wizara ilipangiwa kukusanya shilingi trilioni 1.41, lakini hadi Machi 2026 tayari shilingi trilioni 1.03 zilikuwa zimekusanywa na kuwasilishwa Hazina, sawa na asilimia 114.94 ya lengo la kipindi husika.

Alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na kuimarishwa kwa usimamizi na ukaguzi katika maeneo ya uchimbaji, masoko ya madini, vituo vya ununuzi na mipaka ya nchi ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali.

Aidha, biashara ya madini imeongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo thamani ya mauzo ilifikia shilingi trilioni 4.90 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.82 kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Waziri huyo pia alieleza kuwa Serikali imeendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini, ambapo madini yenye thamani ya shilingi bilioni 3.31 yalikamatwa katika matukio 55 na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wa mapato ya fedha za kigeni, sekta ya madini imeendelea kuimarika ambapo mwaka 2025 mauzo ya madini nje ya nchi yalifikia dola milioni 5,401.9 kutoka dola milioni 4,119.9 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 31.1.


Aliongeza kuwa mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024 na kufikia wastani wa asilimia 11.9 katika robo tatu za mwaka 2025.

Kwa ujumla, Wizara ya Madini imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali, kuongeza uwekezaji na kuendeleza mnyororo wa thamani ya madini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania.

No comments:

Post a Comment