SERIKALI YA RAIS SAMIA YAENDELEA KUNG’ARA KATIKA KUVUTIA UWEKEZAJI WA MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 27, 2026

SERIKALI YA RAIS SAMIA YAENDELEA KUNG’ARA KATIKA KUVUTIA UWEKEZAJI WA MADINI


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, hususan katika sekta ya madini ambayo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, alisema mafanikio hayo yametokana na sera thabiti na mageuzi mbalimbali yaliyolenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Alisema kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Fraser ya Canada wa mwaka 2025, Tanzania imepanda hadi nafasi ya nne Afrika na ya 34 duniani katika kiashiria cha kuvutia uwekezaji, ikiwa imeongeza alama hadi 68.04 kutoka 62.75 mwaka 2024.

Mbali na hilo, Tanzania imeendelea kuimarika katika hazina ya rasilimali madini duniani kwa kushika nafasi ya 15, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa nchi zenye fursa kubwa za uwekezaji katika sekta hiyo.

Mhe. Mavunde alieleza kuwa sekta ya madini imeendelea kuongoza kwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI), ambapo mtaji umeongezeka kutoka dola bilioni 8.64 mwaka 2022 hadi kufikia dola bilioni 9.79 mwaka 2024.

Alibainisha kuwa ongezeko hilo limechangiwa na juhudi za Serikali katika kuhamasisha uwekezaji, kuboresha mazingira ya biashara, pamoja na kupanua miradi iliyopo na kuvutia uwekezaji mpya.

Katika hatua nyingine, Serikali imefanikiwa kusaini mikataba ya miradi mikubwa ya kimkakati ya madini ikiwemo mradi wa niobium wa Panda Hill uliopo mkoani Mbeya, uliosainiwa Machi 24, 2026.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo unatarajiwa kuiweka Tanzania katika nafasi ya wazalishaji wakubwa wa madini ya niobium duniani, sambamba na kutoa ajira zaidi ya 1,600 za moja kwa moja na maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja.

Aidha, Serikali inatarajia kunufaika kwa mapato makubwa yatokanayo na kodi, mrabaha na gawio la hisa, ambapo zaidi ya shilingi trilioni 2 zinatarajiwa kupatikana kupitia mradi huo.

Kwa ujumla, mafanikio haya yanaonyesha mwelekeo chanya wa sekta ya madini nchini na kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji na uchumi imara barani Afrika.

No comments:

Post a Comment