WIZARA YA MADINI YAOMBA BILIONI 174.9 KUTEKELEZA BAJETI 2026/2027 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 27, 2026

WIZARA YA MADINI YAOMBA BILIONI 174.9 KUTEKELEZA BAJETI 2026/2027


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA 


Wizara ya Madini imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 174.98 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake pamoja na kufikia malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya zaidi ya shilingi trilioni 1.4.

Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, alisema fedha hizo zitaiwezesha wizara pamoja na taasisi zake kuendelea kusimamia sekta ya madini kwa ufanisi na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Alieleza kuwa kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 71.51 sawa na asilimia 40.87 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayolenga kukuza sekta hiyo na kuongeza thamani ya rasilimali madini nchini.

Kwa upande wa matumizi ya kawaida, wizara imepanga kutumia shilingi bilioni 103.47 sawa na asilimia 59.13 ya bajeti yote, ikiwa ni pamoja na kugharamia shughuli za kila siku za uendeshaji wa wizara na taasisi zake.

Mhe. Mavunde alibainisha kuwa ndani ya fedha za matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 27.36 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, huku shilingi bilioni 76.11 zikielekezwa kwenye matumizi mengineyo ya kiutendaji.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo utawezesha kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli unaolengwa kufikia shilingi trilioni 1.406, sambamba na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali madini nchini.

Aidha, alisema wizara itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kupitishwa kwa bajeti hiyo kutatoa fursa zaidi kwa sekta ya madini kuendelea kukua na kuwa chanzo kikuu cha mapato ya Serikali na fedha za kigeni.

Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha fedha zitakazoidhinishwa zinatumika kwa ufanisi na uwajibikaji mkubwa ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment