Mkutano Maalumu wa 60 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeridhia mapendekezo ya bajeti ya Sekretarieti ya Jumuiya pamoja na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, katika kikao kilichofanyika Mei 22, 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri na viongozi waandamizi kutoka Nchi Wanachama wa EAC, ikiwa ni hatua ya muhimu ya maandalizi ya Bajeti ya Jumuiya kabla ya kuwasilishwa katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya Juni 30, 2026.
Kabla ya mkutano huo wa Mawaziri, vilifanyika vikao vya ngazi ya wataalamu kuanzia Mei 18 hadi 20, 2026, kikifuatiwa na kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika Mei 21, 2026, hatua ambazo zililenga kupitia na kuboresha mapendekezo ya bajeti kabla ya kuwasilishwa kwa Baraza la Mawaziri.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Mkutano huo, Bi. Edith Mwanje, alisema kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa malengo ya Jumuiya kupitia vipaumbele vilivyoainishwa katika mapendekezo ya bajeti hiyo.
Aliongeza kusema kuwa, mapendekezo ya bajeti yaliyowasilishwa yamezingatia maelekezo yaliyotolewa na Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa EAC, ikiwemo kushughulikia changamoto za kifedha zinazoikabili Jumuiya kama vile ulipaji wa malimbikizo ya mishahara ya watumishi, malipo kwa watoa huduma, pamoja na kuajiri watumishi wapya ili kuongeza ufanisi wa Sekretariati na Taasisi zake.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, akiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya; Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa; pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.












No comments:
Post a Comment