
Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amewaeleza wananchi kuwa Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa Barabara ya Bugene - Burigi Chato (Km 60) kwa kiwango cha lami anaendelea na kazi, ambapo ameshuhudia mkandarasi huyo akiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha kazi ya kukata maeneo korofi ya barabara yaliyokuwa na milima.
Bashungwa ameeleza hayo leo, tarehe 16 Mei 2026 wilayani Karagwe katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi na barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambapo alitembelea na kukagua ujenzi wa Barabara ya Bugene - Burigi Chato inayoelekea Benaco wilayani Ngara.
“Sasa hivi ninasukuma, nafuatilia na kuitaka Serikali, katika kipande cha barabara hii cha Bugene - Burigi Chato ambacho mkandarasi yupo site kikamilike, na nimetoka kuikagua. Mkandarasi kuna hela anadai lakini habari njema ni kuwa kutoka Nyakahanga - Nyaishozi - Chabalisha hadi Kijiji cha Muungano kazi ya kukata milima wapo wanakamilisha.”
Akiwatoa hofu wananchi kutokana na kasi ndogo ya Mkandarasi wa mradi huo, Bashungwa amesema kuwa hatua ya mkandarasi kumalizia kazi katika maeneo korofi ni hatua itakayomwezesha kuongeza kasi ya utekelezaji, kwani maeneo hayo yapo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Bashungwa ameeleza kuwa anaenda kufuatilia malipo anayodai mkandarasi huyo ili kuwezesha kuongeza kasi ya utekelezaji wa barabara hiyo ambayo mpaka sasa imefikia asilimia 48 ya utekelezaji.
Aidha, Bashungwa ameeleza mipango mingine ya kuunganisha barabara hiyo na maeneo mengine ya Bushangaro kupitia maeneo ya Chanyamisa, Nyaishozi, Bisheshe na Nyakahanga
Katika Barabara ya Nyakahanga - Nyakaiga, Bashungwa ameeleza kuwa barabara hiyo imekuwa ikiwekewa lami katika maeneo korofi, kufikia mwakani mkandarasi ataanza kujenga lami kuanzia eneo la Nyakahanga kuelekea Omurusimbi, ambapo ujenzi wa barabara hiyo utaambatana na uwekaji wa taa za barabarani.
Kadhalika, ameeleza mpango wa TANROADS kwa kushirikiana na TARURA kufanya usanifu wa kuweka lami katika maeneo ya mjini (center) katika eneo la Nyakaiga na maeneo mengine ya mji yanayoendelea kukua pamoja na kufunga taa za barabarani katika maeno ya Center za Rwambaizi na nyaishozi.
Bashungwa amewaeleza wananchi kuwa yale yaliyoelezwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Mwenyekiti wake na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan sasa ni kipindi cha utekelezaji na kuhakikisha yale yaliyoahidiwa yanatekelezwa.







No comments:
Post a Comment