NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SERIKALI imewataka vijana nchini kutumia ubunifu, ujuzi na teknolojia kama nyenzo muhimu za kuchochea ukuaji wa biashara, viwanda na ajira, ikisisitiza kuwa maendeleo ya uchumi wa taifa yanategemea uwekezaji katika rasilimali watu wenye maarifa ya vitendo na uwezo wa kuzalisha thamani.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 29, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, wakati akizungumza katika kilele cha Wiki ya Ukuaji katika Kazi na Bunifu za Biashara kwa Vijana (Career Fair 2026) kilichoandaliwa na College of Business Education (CBE).
Akizungumza katika tukio hilo lililobeba kaulimbiu ya “Ubunifu na Ujuzi kwa Vijana; Msingi wa Ukuaji wa Biashara na Viwanda Tanzania,” Londo amesema dunia ya sasa haihitaji vijana wenye vyeti pekee bali wenye maarifa ya vitendo, ubunifu, nidhamu ya kazi na uwezo wa kutumia teknolojia kujenga ushindani katika soko la ajira na biashara.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uzalishaji, biashara, ujasiriamali na maendeleo ya viwanda kupitia sera na programu mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi.
“Tunasisitiza ukuzaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika mnyororo wa thamani wa viwanda kupitia elimu ya ujasiriamali, teknolojia, mitaji na masoko,” amesema.
Aidha, amesema katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika elimu, ubunifu, teknolojia na ujasiriamali ili kujenga uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu ulio jumuishi, himilivu na wenye ushindani.
Londo amesema sekta binafsi, hususan biashara za ubunifu zinazoendeshwa na vijana, zina nafasi kubwa katika kuongeza ajira, kukuza kipato cha wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Katika hatua nyingine, ameipongeza CBE kwa kuandaa Career Fair 2026 akisema jukwaa hilo limekuwa daraja muhimu linalounganisha elimu, soko la ajira, biashara na viwanda kwa kuwapa vijana nafasi ya kujifunza kutoka kwa wataalamu, kuonesha bunifu zao, kupata taarifa za fursa na kujenga mitandao ya kitaaluma.
Naibu Waziri huyo amesema ameridhishwa na mafanikio ya CBE baada ya kushika nafasi ya 10 katika ubora wa vyuo vya elimu ya juu nchini, akieleza kuwa tafiti zinazochapishwa katika majarida ya kitaifa na kimataifa zimechangia mafanikio hayo.
Sambamba na hilo, ameipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa jengo la metrolojia lililofikia asilimia 99 ya utekelezaji katika awamu ya kwanza pamoja na maendeleo ya kampasi mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CBE, Zakaria Mganilwa, amesema chuo hicho kitaendelea kuimarisha ubora, uwajibikaji na ushirikiano na wadau ili kuhakikisha programu zake zinajibu mahitaji ya taifa katika sekta za biashara, ujasiriamali, usimamizi, fedha, teknolojia na stadi za kazi.
Amewahimiza vijana kuitumia Career Fair kama jukwaa la kujitambua na kutafuta fursa za kujiajiri, kubuni bidhaa na huduma, kutumia teknolojia pamoja na kushirikiana na wengine badala ya kusubiri ajira pekee.
Aidha, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kufadhili Mkutano wa Kitaaluma wa Kimataifa wa 9BEDC 2026 utakaofanyika jijini Mwanza Oktoba 22–23, 2026 kwa lengo la kuwasilisha matokeo ya tafiti za kitaaluma kutoka kwa wataalamu wa ndani na nje ya nchi.
Naye Mkuu wa Chuo CBE, Edda Lwoga amesema Career Fair ni sehemu ya juhudi za kuunganisha elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira, biashara na viwanda.
Amesema kupitia jukwaa hilo wanafunzi wanapata fursa ya kusikiliza mada kutoka kwa wataalamu kuhusu maendeleo ya taaluma, sekta ya benki, ujasiriamali, atamizi za biashara, uwezeshaji wa kiuchumi, teknolojia, usajili wa biashara, ubunifu na fursa za ajira.

No comments:
Post a Comment