Na Mwandishi Wetu
Benki ya Ushirika (Coop Bank) mwishoni mwa wiki ilizindua rasmi tawi lake jipya Mtwara mjini ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa benki hiyo wa kupanua huduma za kifedha na kuimarisha uchumi jumuishi.
Kwa uzinduzi huo, mtandao wa matawi ya Coop Bank umeongezeka na kufikia matawi matano ambapo ni Dodoma, Moshi, Tabora, Tandahimba na Mtwara.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo chini ya kauli mbiu “Ustawi Jumuishi, Uwezo kwa memba”, Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Donald Msengi aliishukuru benki hiyo kwa kuendelea kuwa na Imani na mkoa wake huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ilikuvujia uwekezaji zaidi mkoani humo.
“Uzinduzi wa Tawi hili hapa Mtwara mjini ishara tosha ya imani kubwa ambayo Coop Bank inaendelea kuiweka katika mkoa wetu kwa kuwa tayari wana tawi wilayani Tandahimba.” alisema.
Aliongeza, “Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wengi zaidi, hasa vijijini,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Coop Bank Dr. Joseph Witts kupitia hotuba yake iliyosomwa na mjumbe wa Bodi wa Benki hiyo Mohamed Mwinguku alisema uzinduzi wa tawi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpana wa benki hiyo wa kusogeza huduma karibu na wananchi, kwa lengo la kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na ustawi kwa wote.
“Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, hasa kupitia zao la korosho. Kama Bodi, tulifanya uamuzi wa makusudi kuwekeza hapa kwa sababu tunaamini katika uwezo wa wananchi wa Mtwara na fursa zilizopo katika mkoa huu,” alisema.
Dkt. Witts alisema kupitia tawi hilo, Coop Bank itaendelea kutoa masuluhisho ya kifedha yatakayokidhi mahitaji ya wananchi yakiwemo mikopo nafuu, huduma za kidijitali, na ushauri wa kifedha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank Godfrey Ngu’urah alisema benki yake baada ya uzinduzi wa tawi hilo imejipanga kuzindua matawi mengine matatu kabla ya mwisho wa robo ya tatu ya mwaka huu mikoani Dar es Salaam, Kagera na Mwanza.
Ng’urah alibainisha kuwa benki yake imepata mafanikio makubwa ndani ya mwaka mmoja baada ya kuzinduliwa kwake akatumia fursa hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali kwa kuendelea kuwa na Imani na benki yake.
Alibainisha kuwa Kitabu cha mikopo cha benki hiyo kimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 101.02 kutoka shilingi bilioni 16.6, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 506, huku amana za wateja zikifikia shilingi bilioni 101.5 kutoka shilingi bilioni 12.5, sawa na ukuaji wa asilimia 709.
“Fedha za wanahisa zimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 42.1 katika robo ya kwanza ya mwaka huu kutoka shilingi bilioni 27.4 ya robo ya kwanza ya mwaka 2025 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 54,” alisema.
Ng’urah aliongeza kuwa ndani ya mwaka mmoja, benki imeongeza wateja wake hadi kufikia zaidi ya 37,000 kutoka wateja 5,000 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, hatua inayodhihirisha kukua kwa imani ya wateja na kupanuka kwa wigo wa huduma.











No comments:
Post a Comment