WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kupitia ujenzi wa shule za amali na ufundi nchini kote ili kuwawezesha vijana kupata elimu yenye ujuzi na kujitegemea.
Amesema hayo leo Jumamosi, Mei 16, 2026 alipokuwa akikagua ujenzi wa Shule ya Ufundi ya Amali Kingale, Halmashauri ya Mji wa Kondoa mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka minne hadi mitano, Serikali imejenga shule za amali 103 nchini kote ambapo shule 29 kati ya hizo ni za uhandisi, hatua ambayo amesema ni mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu ya ufundi nchini.
“Tangu uhuru tulikuwa na shule tano tu za ufundi, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miaka yake minne hadi mitano amejenga shule 103 za amali, ishirini na tisa zikiwa za uhandisi. Hili ni jambo kubwa sana,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali iliamua kujenga shule hizo kwa nchi nzima kwa wakati mmoja ili kila mkoa unufaike na fursa hiyo ya elimu ya ufundi.
“Alisema kila mkoa upate awamu ya kwanza na watoto waanze kusoma, na baada ya hapo itakuja awamu ya pili ya kumalizia,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuajiri walimu wa sekta za elimu na afya ambapo ndani ya siku 100 pekee walimu 7,000 waliajiriwa wengi wao wakiwa wa masomo ya sayansi.
Pia, Waziri Mkuu amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kunufaika na mpango wa Samia Scholarship unaowawezesha wanafunzi wanaofanya vizuri kupata ufadhili wa masomo ndani na nje ya nchi.
“Ukifanya vizuri sana unapewa Samia Scholarship, huo sio mkopo unapewa fedha ya ufadhili wa kusoma na unachagua chuo chochote duniani,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Saidi Majaliwa amesema shule hiyo ilipokea zaidi ya shilingi milioni 544.2 kupitia Programu ya Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, matundu 10 ya vyoo, jengo la TEHAMA, jengo la utawala, maktaba, majengo mawili ya maabara pamoja na nyumba ya mwalimu. Aidha, shule hiyo ilisajiliwa rasmi tarehe 10 Juni, 2025 ikiwa na walimu sita na wanafunzi 126 wakiwemo wavulana 62 na wasichana 64.
Majaliwa amesema mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa elimu ya ufundi kwa vijana, kuibua vipaji, kuchochea ajira na kujitegemea pamoja na kupunguza umbali wa wanafunzi kufuata mafunzo ya ufundi.






No comments:
Post a Comment