
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent Luoga amekutana na Naibu Balozi wa New Zealand nchini, Nicholas Meehan ambapo wamejadiliana kuhusu ushirikiano katika miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia rasilimali ya jotoardhi.
Kikao hicho kimefanyika leo, tarehe 4 Mei 2026, katika Ofisi za Wizara ya Nishati Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Luoga ameishukuru Serikali ya New Zealand kwa mchango wake katika miradi ya jotoardhi nchini kupitia programu ya Africa Geothermal Facility (AGF1) awamu ya kwanza iliyowezesha watumishi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) kujengewa uwezo wa kiufundi na kitaasisi, jambo lililowaongezea ujuzi wa kuendeleza kazi zao kwa weledi zaidi.
Anesisitiza kuwa mradi wa AGF1 awamu ya kwanza umefika tamati lakini Tanzania inahitaji ushirikiano huo uendelee ili kuendeleza rasilimali ya jotoardhi ambapo Tanzania inalenga kuzalisha takribani MW 130 kutokana na nishati hiyoi ifikapo 2030.
Amefafanua kuwa, Wizara kupitia TGDC imepanga miradi miwili ya kimkakati itakayoweza kufanikisha lengo hilo ambayo ni mradi wa Ngozi utakaozalisha megawati 60 pamoja na Kiejo-Mbaka utakaozalisha megawati 70.
Aidha, ameiomba New Zealand kuangalia uwezekano wa kufadhili miradi hiyo ya kimkakati, pia kusaidia kutafuta ufadhili wa miradi hiyo.
Kwa upande wake, Balozi Meehan ameeleza kuwa New Zealand inatambua ushirikiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili hususan katika miradi ya jotoardhi huku akiahidi kuendeleza ushirikiano kupitia awamu ya pili ya programu ya Africa Geothermal Facility, pamoja na kutafuta nafasi za ufadhili katika masuala ya jotoardhi ili kuwawezesha wataalam wa Tanzania kuongeza weledi na ujuzi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, TGDC, pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.







No comments:
Post a Comment