SEKTA YA VIWANDA YAENDELEA KUKUA, AJIRA ZAIDI YA 25,000 ZAZALISHWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 22, 2026

SEKTA YA VIWANDA YAENDELEA KUKUA, AJIRA ZAIDI YA 25,000 ZAZALISHWA

Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Sekta ya viwanda nchini imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika ukuaji wa uchumi huku ikizalisha maelfu ya ajira na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, ambapo ukuaji wa sekta hiyo umefikia asilimia 5.2 mwaka 2025 kutoka asilimia 4.9 mwaka 2024.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Kapinga amesema pamoja na mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kushuka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2024 hadi asilimia 5.9 mwaka 2025, serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuhamasisha uongezaji thamani wa mazao na rasilimali za nchi.

Amesema katika sekta ya saruji, Tanzania kwa sasa ina viwanda 15 vyenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 13.6 kwa mwaka, huku hadi Aprili 2026 viwanda hivyo vikiwa vimezalisha tani milioni 10.3 dhidi ya mahitaji ya ndani ya tani milioni 8.5 kwa mwaka.

“Uzalishaji huu umeiwezesha Tanzania kuuza ziada ya saruji katika nchi jirani zikiwemo Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi,” amesema Waziri Kapinga.

Aidha, amesema viwanda vya sukari nchini vinaendelea kuimarisha uzalishaji ambapo viwanda saba vya sukari vina uwezo wa kuzalisha tani 800,000 kwa mwaka, huku hadi Aprili 2026 vikiwa vimezalisha tani 410,979 wakati mahitaji ya ndani ni tani 550,000 kwa mwaka.

Katika sekta ya korosho, Waziri Kapinga amesema Tanzania ina viwanda 70 vya kubangua korosho, ambapo viwanda 50 vinafanya kazi na vina uwezo wa kubangua tani 108,549 kwa mwaka. Amesema hadi Aprili 2026 viwanda hivyo vilikuwa vimebangua tani 53,125 za korosho sawa na asilimia 8.6 ya uzalishaji wote wa korosho ghafi nchini.

Kwa upande wa dawa na vifaa tiba, amesema Tanzania ina viwanda 14 vya kuzalisha dawa za binadamu na vifaa tiba ambavyo kwa sasa vinakidhi asilimia 20 ya mahitaji ya dawa nchini, huku serikali ikilenga kuongeza uwezo huo hadi asilimia 60 ifikapo mwaka 2035.

Waziri Kapinga amesema katika mwaka 2025/2026 jumla ya viwanda 11 vipya vya dawa na vifaa tiba vilijengwa na kuanza majaribio ya uzalishaji, vikitoa uwezo wa kuzalisha vizio bilioni 3.5 vya dawa pamoja na kutoa ajira zaidi ya 25,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Liganga, Mchuchuma na Maganga Matitu sambamba na kuimarisha matumizi ya teknolojia na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment